Home » » DKT.DIMWA: AFUNGUA MAFUNZO YA MABALOZI WA MASHINA.

DKT.DIMWA: AFUNGUA MAFUNZO YA MABALOZI WA MASHINA.

Written By CCMdijitali on Thursday, December 12, 2024 | December 12, 2024

Na Is-haka Omar,Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amewataka mabalozi wa mashina ya CCM nchini kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa umakini, ufanisi, na ueledi, kwa kuhakikisha wanachama wote wenye sifa za kupiga kura wanaandikishwa katika zoezi la awamu ya pili la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, linalotarajiwa kufanyika mwezi Februari, mwaka 2025.

Wito huo aliuatoa wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo mabalozi wa CCM Wilaya ya Amani, yaliyofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini, Amani, Zanzibar.

Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinafanya siasa za kisayansi zinazozingatia takwimu halisi za wanachama wake, ili kupata tathmini sahihi inayotoa muelekeo chanya katika kuhakikisha ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Alisema kuwa mabalozi hao wana jukumu kubwa la kufahamu kiwango cha mtaji wa chama katika maeneo yao na kuhamasisha wafuasi wa vyama vingine kujiunga na CCM.

Katika maelezo yake, Dkt. Dimwa pia alikumbusha kuwa CCM ilifanya majaribio ya mitambo yake kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, ambapo ilipata ushindi mkubwa wa zaidi ya asilimia 99.

Aliongeza kuwa hakuna chochote kinachoweza kuzuia CCM kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Mnapewa mafunzo haya kwa ajili ya kuwakumbusha majukumu yenu sambamba na kuwaandaa kisaikolojia kuelewa kuwa wakati wa kupambana katika vita ya kisiasa umefika.
Ni lazima mfanye kazi kwa kujiamini, uzalendo, ukweli, na kufuata maelekezo kutoka kwa viongozi wenu,” alisema Dkt. Dimwa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutekeleza kwa ufanisi ibara ya 5 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 (toleo la 2022), inayoelekeza kuwa ushindi wa CCM ni lazima kwa kila uchaguzi uwe wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa dola. 

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Amani, Getrude Bonifasi, alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji mabalozi hao, ambao ni nguzo muhimu katika upatikanaji wa ushindi wa chama katika kila uchaguzi.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza katika ufunguaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo mabalozi wa mashina ya CCM Wilaya ya Amani(hawapo pichani) yaliyofanyika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani Zanzibar.


BAADHI ya Mabalozi wa mashina wakisikiliza na kufuatilia hotuba ya mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji mabalozi hao yaliyofanyika ukumbi wa CCM Mkoa Mjini uliopo Amani Zanzibar.


Mwisho   

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link