Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewapongeza na kuwashukuru madaktari kutoka hospitali ya MIOT ya India kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia Wazanzibari hasa wagonjwa wa moyo, saratani na kiharusi.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na uongozi wa hospitali hiyo ya MIOT ya Chinnai, India wakiongozwa na mwenyeji wao Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji wakuu wa Wizara ya Afya, Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amepongeza pia uhusiano mzuri uliopo baina ya hospitali hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na kueleza kuwa kuwepo kwao kumeongeza tija kubwa kwa jamii ya Wazanzibar wenye mahitaji ya huduma zao.
Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwepo kwa madaktari hao nchini, ni fursa nzuri kwa wataalamu wa ndani kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo, utaalamu pia kupunguza gharama kubwa kwa wagonjwa wanaopata matibabu kutoka taasisi hiyo.
Naye, Mkurugenzi wa hospitali hiyo ya MIOT, Dk. Prithvi Manawng Mohandas amemueleza Rais Dk. Mwinyi huduma wanazozitoa kwa wagonjwa wa Zanzibar hasa kwa maradhi ya saratani ni tiba za mionzi (Redio therapy), matibabu ya kikemia (Chemical Therapy) na tiba ya kulenga eneo maalum (targeted therapy) pamoja na matibu ya moyo.
Akizungumzia ugonjwa wa kiharusi Dk. Prithvi amemueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba wanawatibu wagonjwa wa maradhi hayo hasa kwa kuwasaidia kuimarisha na kurejesha uwezo wa viungo vyao kwa kutembea na kufanya shughuli zao za kawaida kwa maisha yao ya kila siku.