MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- ZIARA YA KUTEMBELEA HOSPITALI NA KIWANJA CHA MPIRA- CHAKE CHAKE PEMBA
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa huduma bora za Afya kwa hospitali zote za Unguja na Pemba kwa lengo la kuhakikisha Afya za wananchi zinazidi kuimarika siku hadi siku.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Chake - Chake iliyopo Vitongoji Kisiwani Pemba.
Amesema ameridhishwa na utoaji wa huduma za matibabu kwa wagojwa wanaofika hospitalini hapo ikiwa ni pamoja na kufanyiwa vipimo vyote muhimu na kupatiwa dawa wanazohitaji bila ya usumbufu wowote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema amefarijika kuona kuwa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hio wanapatiwa chakula kwa wakati na ratiba ya chakula hospitalini hapo imepangwa kwa utaratibu maalum unaoendana na mahitaji ya lishe bora kwa afya ya binaadamu na kuutaka Uongozi wa Wizara ya Afya kuhakikisha huduma ya chakula inapatikana kwa wagonjwa wote wanaolazwa katika hospitali zote za Zanzibar.
Mhe.Hemed amesema mpango wa Serikali ni kuzidi kuiboresha Sekta ya Afya kwa kuendelea kujenga hospitali mpya kila Wialya na Mkoa kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma zote muhimu ndani ya Kisiwa cha Pemba na kuwapunguzia gharama wananchi ya kufuata matibabu nje ya Zanzibar.
Amezitaka kampuni zilizopata nafasi ya kutoa huduma hospitalini hapo na hospitali nyengine ndani ya Zanzibar kufanya kazi kwa uaminifu na uweledi wa hali ya juu kwa kuhakikisha huduma zote stahiki zinapatikana kwa wakati bila ya usumbufu wa aina yoyote.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Ndugu KAMIS BILALI ALI amesema Mpango mkakati wa Wizara ya Afya ni kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika kufuata huduma katika hospitali zote nchini.
Bilali amesema hospitali ya Wilaya ya Vitongoji imekuwa ikizalisha gesi tiba mitungi mia mbili (200) kwa siku na kusambazwa katika hospitali zote kisiwani Pemba jambo ambalo limesaidia kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa gesi tiba kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hio kisiwani Pemba.
Amesema kabla ya kufungwa kwa mtambo huo wa kuzalisha gesi tiba hospitali hapo Serikali ililazimika kuagiza huduma hio kutoka sehemu nyengine za Tanzania hali ambayo ilikuwa inahatarisha afya za wagojwa wanaohitaji kupatiwa huduma hio.
Nao wagonjwa wanaofika hospitalini hapo akiwemo Bi. ASHA JUMA ABDALLA na Bwana ABDILAHI JUMA RAJAB wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwawekea mazingira mazuri ya upatikanaji wa huduma za afya Mijini na Vijijini.
Wamesema kuwa wahudumu na madaktari waliopo hospitalini hapo wanatoa huduma bora na dawa zinapatikana kwa wakati sambamba na kupata chakula kwa wakati kwa gonjwa wote wanaolazwa hospitalini hapo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea na kukagua maendeleo ya Ukarabati wa Uwanja wa Mpira wa Gombani kisiwani Pemba na kuridhishwa na hatua ya ujenzi huo uliofikia asilimia 75 % unatarajiwa kumalizika mapema mwezi Machi 2025.
Mhe, Hemed amewataka wakandarasi wa ujenzi wa uwanja huo kuhakikisha wanamalizika kazi ndani ya muda wa makubaliano kwa ubora na viwango vya juu ili kutoa fursa kwa wanamichezo wa kisiwani Pemba kukitumia kiwanja hicho kwa kuchezea ligi kuu ya Zanzibar na michezo mingine ya Kitaifa na Kimataifa.
Ukarabati wa Uwanja huo unatarajiwa kumalizika mwezi machi 2025 ambao utajumuisha viwanja vya nje vitano (5) vya michezo mbali mbali pamoja na sehemu ya kuegesha magari kwa wanamichezo wanaofika uwanjani hapo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikagua na kujionea hali ya upatikanaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Chake – Chake Vitongoji Kisiwani Pemba. |
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
29 / 01 / 2025.