Home » » MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI BANDARI YA SHUMBA MJINI- MKOA WA KASKAZINI PEMBA

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI BANDARI YA SHUMBA MJINI- MKOA WA KASKAZINI PEMBA

Written By CCMdijitali on Thursday, January 9, 2025 | January 09, 2025

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Awamu ya Nane (8) inaendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya Bandari kwa Unguja na Pemba ikiwemo Bandari ya Shumba Mjini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

Ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61ya  Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

 

Amesema kukamilika kwa Bandari ya Shumba Mjini kutapelekea kuimarika kwa huduma za usafiri wa Baharini katika Mkoa wa Kaskazini Pemba kutokana na bandari hio kuwa ni kiungo muhimu kati ya Bandari ya Tanga na Mombasa Kenya jambo litakalo wawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi zaidi.

 

Makamu wa Pili wa Rais amesema Ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini na nyengine zinazojengwa Zanzibar ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 ambao kukamilika kwake kutatoa fursa za ajira kwa wakaazi wa maeneo hayo pamoja na kukua kwa uchumi Mkoano humo.

 

Makamku wa Pili wa Rais amemuagiza Mkandarasi anajenga bandarini hio kuongeza nguvu za utendaji kazi na masaa ya kazi ili bandari hio iweze kukamilika na wananchi waweze kunufaika nayo.

 

Sambamba na hayo amewataka wananchi kuthamini na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Mwinyi za kuwaete maendeleo pamoja na kuhimizana  kudumisha Amani na mshikamano uliopo nchini kwa kutokubali kugawanywa na kuingizwa chuki za kisiasa kwa maslahi ya watu wachache wasioitakia mema Zanzibar.

 

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe.Dkt Khalid Salum Muhammed amesema Wizara yake inaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa barabara, Viwanja vya ndege na Bandari Unguja na Pemba ili kukuza uchumi wan chi.

 

Dkt. Khalid amesema ujenzi wa miundombinu ya bandari ikiwemo bandari ya Shumba Mjini  una lengo la kuimarisha na kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji nchini ambapo Serikali inajipanga kuitanua Bandari ya Mpigaduru kwa kujengwa bandari kwa ajili ya usafiri wa Tax na kujengwa eneo litakalotumika kwa utuwaji wa ndege za baharini jambo litakaloondoa changamoto ya huduma ya usafiri wa majini na nchi kavu.

 

Akisoma Taarifa ya Kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiano na Uchukuzi Dkt HABIBA HASSAN OMAR amesema ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 5 zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo itawanufaisha zaidi wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kukuza uchumi wa Mkoa huo.

 

Dkt. Habiba amesema bandari hio itakuwa na urefu wa mita 45 na upana mita 20 ambayo itatoa huduma kwa abiria zaidi ya mia tisa (900) kwa wakati mmoja, kupokea meli zenye uzito wa GRT 2000 ambazo zitashusha na  kupakia  mizigo bandarini hapo.

 

Amefahamisha kuwa katika kuhakikisha usalama wa watendaji na  watumiaji wa  Bandari ya Shumba Mjini taratibu za kuzungushwa uzio bandarini hapo zimekamilika na ujenzi huo unatarajiwa kuanza muda mfupi ujao.

 



Makamu Wa pili wa rais wa Zanzibar akiweka  Jiwe la Msingi la ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61ya  Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.









Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

 08 / 01 / 2025.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link