Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Tanzania ina thamini mchango mkubwa wa Taifa la Marekani katika maendeleo ya nchi kupitia miradi na program mbalimbali zinazofadhiliwa na nchi hiyo, ukiwemo Mkataba wa Msaada wa dola za Marekani bilioni 1.14, uliosainiwa hivi karibuni kwa ajili kuendeleza sekta mbalimbali.
Dkt. Nchemba, ameyasema hayo Jijini Dodoma, wakati akiagana na Balozi wa Marekani aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle, ambapo walitumia fursa ya kikao hicho kujadili maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani hususan katika sekta za biashara na uwekezaji.
“Ninashukuru kwa msaada wa dola za Marekani bilioni 1.14 uliotolewa na Taasisi za Marekani kupitia Program ya Development Objectives Agreement (DOAG), unaoonesha namna Marekani inavyochangia maendeleo ya nchi yetu, ambapo fedha hizo zitaelekezwa kwenye sekta za afya, elimu, kukuza uchumi na utawala bora, hivyo kuchangia Agenda ya Dira ya Taifa ya 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26. ” alisema Dkt. Nchemba.
Mhe. Dkt. Nchemba alirejea pia shukrani zake kwa Marekani kwa kuipa nafasi Tanzania ya kuboresha masuala kadhaa kupitia Mradi wa Millenium Challenge Corporation (MCC), ili nchi iweze kurejea kwenye mpango mkuu wa maendeleo na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeimarisha kwa kiasi kikubwa misingi ya demokrasia, haki za binadamu, utawala bora pamoja na maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Balozi wa Marekani aliyemaliza kipindi chake hapa nchini, Mhe. Michael Battle, alieleza kuwa Marekani na Tanzania ni washirika wa muda mrefu wa maendeleo na kwamba uhusiano huo umeendelea kudumishwa na kuimarishwa hadi sasa.
Mhe. Balozi Battle, aliyeambatana na Naibu wake Bw. Andrew Lentz, alisema kuwa ushirikiano huo unatarajia kuchukua mwelekeo mpya kwa kuhimiza zaidi biashara na uwekezaji kwa faida ya pande zote mbili hususan kwa kutumia ukanda wa kibiashara wa Bahari ya Hindi pamoja na uwepo wa fursa ya gesi (LNG)..
Aidha, alisema kuwa Marekani inaandaa mpango mpya wa kutumia Sheria ya ukuaji wa fursa Afrika (AGOA) unaolenga kukuza masoko na biashara ndani na nje ya Marekani, ambapo mwelekeo utakuwa ni ushirikiano wa kibishara kati ya nchi na nchi (bilateral) badala ya Marekani na Mataifa mengi kwa pamoja (Multilateral).
Mazungumzo ya kuagana na Balozi wa Marekani aliyemaliza muda wake nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle, yalimhusisha pia Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban, Kaimu Mratibu wa Program za Millenium Challenge Corporation-Tanzania (MCC), Dkt. Muhajir Kachwamba, Viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki