• Tanzania, Rwanda na Uganda zakubaliana kusaini hati ya makubaliano ya ujenzi wa Kufua Umeme Nsongezi wa 39MW
Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la Jumuiya ya Afrika Mashariki umeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukamilisha maandalizi ya Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakayofanyika tarehe 5 hadi 7 Machi 2025 jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimetolewa kwenye mkutano wa Baraza hilo uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha.
Uenyeji wa Tanzania katika Kongamano hilo unatokana na Maamuzi ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati uliofanyika Februari 14, 2024 ambao uliamua Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na maonesho hayo.
Kongamano na Maonesho hayo ni mkakati unaolenga kutangaza fursa zilizopo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu rasilimali za mafuta na gesi asilia na kuielezea jiolojia ya ukanda wa Afrika Mashariki ili kuvutia uwekezaji, kuendelezaji wa miundombinu, udhibiti wa uharibifu wa mazingira, usimamizi wa taarifa za mafuta na gesi asilia.
Pia linalenga kutangaza maeneo mapya ya utafutaji na kutangaza maendeleo yaliyopatikana katika sekta ya nishati katika ukanda.
Malengo mengine ni kubadilishana uzoefu kuhusu sera, sheria, kanuni na utaalamu unaotumika kwenye sekta ya nishati, kuhamasisha uwekezaji, utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia. Vilevile Kongamano hilo linatoa fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kongamano na maonesho hayo yanatoa fursa adhimu kwa Tanzania kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya Nishati hususan katika sekta ndogo ya mafuta na gesi na hivyo kuongeza wigo wa kupata wawekezaji kwenye sekta hiyo.
Mbali na hayo, Mkutano 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC limepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali katika sekta ya nishati, petroli na madini ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Nsongezi wenye Megawati 39 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera utakaotelezwa kwa pamoja baina ya Tanzania, Rwanda na Uganda.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini uliongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde (Mb.), Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (Mb.), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi- Zanzibar Bw. Zahor Alharousy na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC uliofanyika jijini Arusha |
Meza Kuu wakiongoza mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliokuwa ukiendelea katika Makao Mkuu ya Jumuiya jijini Arusha. |
![]() |
Ujumbe wa Tanzania, Uganda na Rwanda wakionesha hati ya makubaliano (MOU) ya ujenzi wa Kufua Umeme wa Nsongezi 39MW. |