Na Maelezo Zanzibar 17/02/2025
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George J. Kazi amewataka wananchi waliofikia umri wa kupiga kura kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili kupata haki yao ya msingi.
Jaji Kazi ameyasema hayo katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar katika mkutano na wadau kuhusu Uandikishaji wapiga kura wapya wa awamu ya pili.
Amesema kila mwananchi aliyefikia umri wa mika 18 ana haki ya kuandikisha katika daftari la wapiga kura na kufuata vigezo vya kuwa mpiga kura
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa jumla ya wapiga kura wapya 78922 nchini wanaokadiriwa kuandikishwa katika daftari la wapiga kura kwa mujibu wa takwimu za sensa ilifanyika 2022.
Amesema zoezi la uandikishaji wapiga kura wapya awamu ya Pili limeshakamilika kisiwani Pemba ambapo zoezi limefanyika kwa Amani na utulivu kwa wananchi wenye sifa walipata haki yao hiyo ya msingi.
Ameeleza kuwa upande wa Unguja zoezi hilo linatarajiwa kuanza tarehe 22 mwezi huu huko wilaya Kaskazini ‘A’ na kumalizika tarehe 17 mwezi wa Machi katika Wilaya ya Mjini.
Aidha Jaji Kazi amewasisitiza wanasiasa kuacha kutumia kauli za uchochezi na viashiria vya uvunjifu wa amani ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa Amani na utulivu na kuwakilisha wakala wao katekeleza majukumu yao.
Akitoa Mada kuhusu Taarifa na Utaratibu wa uandikishaji wa wapiga kura awamu ya pili na uendeshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2025 Mkurugenzi Tume ya Uchaguzi Thabit Idarous Faina amesema uandikishaji wapiga kura wapya utafanyika katika vituo vilivyotangazwa na Tume mbele ya mawakala wa uandikishaji na kila mwananchi atakaefika kituoni kuomba kuandikishwa atawasilisha kitambulisho cha Mzanzibar mkaazi kwa karani muandikishaji.
Nae mwasilishaji kutoka Kurugenzi ya Huduma za sharia Ndugu Maulid Ame Mohamed amesema uandikishaji na uendelezaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Zanzibar umeainishwa na kufafanuliwa katika kifungu cha 7(1) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kimetoa haki kwa kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 kupiga kura kwa uchaguzi unaofanyika Zanzibar.
Amefafanua kuwa kifungu hicho kinaeleza kuwa Kila mzanzibar aliyemitiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Zanzibar na wananchi na haki hiyo itatumiwa kwa kufuata masharti ya kifungu cha (2) cha kifungu hicho pamoja na masharti mengine Katika hayo nayo ni sheria inayotumika Zanzibar kuhusu mambo ya uchaguzi.
Nao washiriki wa mkutano huo wameomba watu wenye kupatiwa mazingira rafiki na kuzingatia uwiano katika zoezi hilo pamoja na wamesisitiza kudumisha katika kipindi chote cha uandikishaji hadi kufikia uchaguzi mkuu.
Akifunga mkutano Makamu mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Aziza Iddi Suweid amewataka wadau hao kuhamasisha jamii kuhusiana na zoezi zima la uandikishaji pamoja na kuvisisitiza vyombo vya habari kusikiliza na kufuata utaratibu uliowekwa na Tume ya Utangazaji katika kutoa taarifa kipindi chote cha uchaguzi ili kwenda sambamba sharia zilizowekwa na Tume hiyo.
Mkutano huo umewashirikihsa wadau mbalimbali wa Uchguzi vikiwemo vyombo vya Usalama, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, vyama vya siasa, asasi za kiraia, watu wenye ulemavu pmoja na taasisi za habari wenye kauli mbiu "Kura haki yako, Amani wajibu wako’’