Makatibu Wakuu wanaosimamia Sekta ya Nishati, Petroli na Madini katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC kujadili masuala muhimu ya pamoja yanayohusu sekta hizo.
Mkutano huo pamoja na musuala mengine umepokea na kujadili ripoti ya maendeleo ya sekta ya nishati ya umeme, petroli, madini na nishati jadidifu iliyotokana na mkutano wa Wataalam uliyofanyika tarehe 10 -12 Februari 2025.
Miongoni mwa taarifa iliyojumuisha kwenye ripoti hiyo ni pamoja na; taarifa ya hali ya upatikanaji na hatua iliyofikiwa kwenye usambazaji wa nishati ya umeme katika nchi wanachama, na utelekelezaji wa miradi ya pamoja ya kuzalisha na kusambaza umeme ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme kwa nguvu za maji wa Nsongezi wa 39MW unaotarajiwa kutelezwa kwa pamoja baina ya nchi ya Tanzania, Rwanda na Uganda
Mbali na hayo mkutano huo unalenga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kupitia miradi na programu mbalimbali ilikuongeza ufanisi katika maeneo muhimu ikiwemo upatikanaji na usambazaji, usimamizi na utafutaji wa rasilimali hizo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa wananchi na kuleta tija zaidi katika ukuaji wa maendeleo ya kijamii na uchumi wa Jumuiya.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki katika Jamhuri ya Kenya Bw. Abdi Dubati ameeleza kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za Wakuu wa Nchi wanachana wa Jumuiya, za kuhahikisha sekta ya nishati inaimarika ili kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya.
“Wote tunatambua kuwa sekta ya nishati, petrol na madini zinamchango wakipekee katika maendeleo ya uchumi wa Jumuiya yetu, hivyo nitoe rai kwetu sote kwa umoja wetu kutumia fursa hii na utaalamu wetu katika kuhakikisha wananchi wetu wanapata nishati ya uhahikika kwa bei nafuu huku tukitilia mkazo zaidi kwenye kutafuta na kuhimiza matumizi yanishati mbadala”. Alisema Dubati.
Mkutano huo wa ngazi ya Makatibu Wakuu ni Maandalizi ya Mkutano wa 17 wa Mawaziri wa Nishati, Petroli na Madini unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 14 Februari 2025 katika Makao Makuu ya Jumuiya ya EAC jijini Arusha.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo Ngazi ya Makatibu Wakuu ulijumuisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi- Zanzibar Bw. Zahor Alharousy, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahaya Samamba, ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi.
![]() |
Meza Kuu wakiongoza mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliokuwa ukiendelea katika Makao Mkuu ya Jumuiya jijini Arusha. |