Home » » MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI ZMA YAJADILI KANUNI MPYA ZA MICHEZO YA BAHARINI 2025

MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI ZMA YAJADILI KANUNI MPYA ZA MICHEZO YA BAHARINI 2025

Written By CCMdijitali on Thursday, February 13, 2025 | February 13, 2025

 Mratibu wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Nd.Juma Vuai Mbarouk amewataka wadau husika kuwashirikisha katika hatua ya mwanzoni ya kupokea maoni na kanuni mpya ya michezo ya Baharini iliyotayarishwa na Mamlaka inayotarajiwa kukamilika mwaka huu wa 2025 kwa dhamira ya muongozo wa uendeshaji, utaratibu na usimamizi wa shughuli za michezo ya Baharini.


Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao ambacho kilifanyika leo Makunduchi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkoa wa Kusini Unguja.


“ Zanzibar imekuwa na ongezeko la Watalii kutokana na utulivu wa Nchi yetu, miundombinu bora, kuongezeka kwa vivutio vya Utalii, jambo ambalo linapelekea hata michezo ya Baharini kuongezeka katika maeneo mbalimbali ya fukwe zetu”. Amesema Mratibu.


Amesisitiza kuwa michezo inakuwa kwa kasi na maarufu katika fukwe mbalimbali za visiwani kama fukwe za Kendwa, Nungwi Pwani Mchangani, Kiwengwa, Paje, Jambiani maeneo mengineyo yanayohusisha michezo ya pikipiki Baharini Michezo ya parachuti, vishada vinavyovutwa na upepo ama boti michezo kuelea Baharini kwa boti ndogo zisizo za mbao na  kupanda Farasi Baharini.


Vile vile ameongeza kuwa kwa muda mrefu shughuli hizo zilikuwa zikitekelezwa bila ya kuwepo muongozo rasmi wa usimamizi wa michezo jambo ambalo lilipelekea kuibua kwa migogoro tofauti baina ya wadau wanaojishughulisha na michezo hiyo na kuhatarisha usalama wa Nchi.


Hata hivyo Mratibu alieleza kwamba kutungwa kwa kanuni hiyo ni jitihada za kutaka kuhakikisha michezo ya Baharini inaibuka na kuimarika kwa kasi visiwani na inafanyika kwa usimamizi na udhibiti wenye ufanisi kwa kuainisha maeneo husika ili kutatua migogoro ya matumizi ya fukwe, kusimamia usalama wa shughuli husika na bila kusahau kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa Serikali.


Nae muwasilishaji  wa muundo wa  kanuni  Afisa kutoka Mamlaka ya Usafiri Baharini bi Zuhura Khamis Rajab amesema  kanuni ya michezo Baharini ya mwaka 2025 iliundwa chini ya kifungu 491 cha sheria ya usafiri Baharini ya namba 6 mwaka 2009 na iliundwa kanuni hiyo kwa sura ya 12 zilizojumuisha sambamba na kanuni 69.


Aidha amesema kwamba madhumuni ya kanuni hiyo itasaidia  Mamlaka kuwa na nguvu za kisheria na kuweka utaratibu mzima wa usimamizi na uendeshaji udhibiti wa aina zote za michezo Baharini katika maeneo ya michezo ya uratibu na mipaka ya uendeshaji wa michezo hiyo.


Kwa upande wa wadau kutoka sehemu tofauti tofauti  wakitoa maoni yao mbele ya kikao hicho walisema changamoto kubwa inayowasumbua ni utitiri wa kodi kwa hiyo wanaiyomba Serikali iweke leseni moja ili waweze kulipia kwa wakati.


Wadau hao walieleza pia Taasisi inayohusika na masuala mazima ya usafi wahakikishe wanaweka utratibu mzuri wa kuweka mazingira safi hasa katika fukwe.


Kikao hicho ni cha siku moja ambacho kiliwashirikisha Maafisa kutoka ZMA, wadau mbali mbali kutoka  coconuts Kite Jambiani Mbuzi Kite Center n.k na kikao hicho kughairishwa na Mratibu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.


















Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link