Home » » Mawaziri EAC na SADC wakutana Dar kujadili mzozo DRC

Mawaziri EAC na SADC wakutana Dar kujadili mzozo DRC

Written By CCMdijitali on Friday, February 7, 2025 | February 07, 2025



Na Grace Semfuko, Maelezo. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, wamekutana Leo Februari 07, 2025 jijini Dar es Salaam, kujadili mzozo wa Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikao cha Marais wa jumuiya hizo, kitakachofanyika Kesho Jumamosi Februari 8, 2025. 

Lengo la kikao hicho ni kutafuta suluhu ya mzozo mjini Goma, Mashariki mwa DRC. 

Kikao hicho kimeongozwa na Wenyeviti wawili akiwepo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Veronika Mueni Nduva, na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi, pamoja na wenyeviti wenza Mhe. Musalia Mudavadi Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, na Profesa Amon Murwira Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe. 

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania inaunga mkono juhudi za EAC na SADC, za kutaka suluhu nchini Congo DRC na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wa kuwa mwenyeji wa kikao hicho kwa manufaa ya ukanda wa nchi hizo. "Hiki ni kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ni kikao cha maandalizi ya kikao cha wakuu wa nchi kitakachofanyika Febriari 08, ni matumaini yangu kikao hiki kitakuwa na mafanikio, na hapa naomba nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maamuzi yake ya kuwa mwenyeji wa kikao hiki" amesema Balozi Kombo.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho kutoka Jumuiya ya Afrika- EAC Mashariki Mhe. Veronika Mueni Nduva, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo amesema usalama wa DRC ni muhimu sana kwa maendeleo ya jumuiya, hivyo anaamini jitihada za EAC na SADC zitaleta matunda mazuri.

 “Kinachoendelea DRC inahitaji tuwe wamoja, hali hii inagusa kila mtu, usalama wa DRC ni muhimu sana kwa maendeleo ya jumuiya yetu na ukanda wote kwa ujumla, naamini jitihada zetu hizi zitaleta matunda mazuri" amesema Mhe. Nduva. 

Nae Mwenyekiti mwenza wa kikao hicho kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Mhe. Elias Magosi amesema, ni lazima maamuzi ya dhati yachukuliwe ili kutatua mzozo huo na kurudisha Amani na mshikamano DRC. 

“Ni lazima tuchukue maamuzi kurudisha Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vita imegharimu maisha ya watu wengi, wanawake na watoto wanataabika, hali hii ikiendelea kutakuwa na madhara makubwa, natoa wito kwa sehemu zinazohusika na mgogoro huokusitisha na kufanya mazungumzo" amesema Mhe. Magosi. 

Kikao hicho kinalenga kuleta suluhu ya mgogoro huo, huku kikiwataka wahusika kuweka silaha chini na kufanya mazungumzo ya Amani, ambapo kesho Februari 08, 2025, Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), watakutana Jijini Dar es Salaam kujadili suluhu ya mzozo huo.




Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link