Waziri Ofisi ya waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa serikali itaendelea kufanya tathimini ya kupima uhimilivu wa Mifuko kila baada ya miaka mitatu kama inavyoelekezwa kisheria ili kuangalia uwezo wa kuboresha mafao bila kuathiri uendelevu wake.
Amesema hayo leo Februari 10, 2025 Bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Mhe. Nicodemas Henry Maganga (Mb) aliyetaka kujua ni lini Serikali itafanya mabadiliko kwenye kikokotoo cha Watumishi nchini.
Akijibu swali hilo, Mhe. Ridhiwani amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 serikali ilifanya mabadiliko ya Kikokotoo kwa watumishi nchini na mwaka 2024/2025 imefanya maboresho zaidi kwenye kikokotoo hicho baada ya mjadala ndani ya Bunge.
Vile vile, amesema maeneo yaliyofanyiwa maboresho zaidi ni pamoja na malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 kwa waliokuwa wanalipwa asilimia 50, na kutoka asilimia 33 hadi 35 kwa waliokuwa wanapata asimilia 25 kabla ya kuunganisha Mifuko mwaka 2018.
Pia, amesema Januari 2025, Serikali imeongeza kima cha chini cha pensheni kutoka sh. 100,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani amesema serikali imehuisha pensheni ya kila mwezi kwa kiwango cha asilimia mbili kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.