Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wajumbe kuchagua wagombea watakaoweza kuwasikiliza changamoto zao na kuzichukulia hatua.
Ameyasema hayo alipokutana na Viongozi wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Kamati za Siasa za Jimbo na wadi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama ndani ya Wilaya ya Amani, Mkoa wa Mjini kichama kwenye Ukumbi wa CCM Amani Mkoa.
Amesema wakati umefika kwa wana CCM kuchagua wagombea wenye nia thabiti ya kukitumikia chama na wananchi wake na sio kuchagua mtu mwenye kipato ama umaarufu ambae hatoweza kuwatumikia.
Mhe. Hemed amevitaka vikao vya maamuzi kufuata matakwa ya katiba ya chama kwa kufanya haki na uadilifu wakati wa kupitisha wagombea ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima ndani ya chama na kwenye jamii itakayopelekea mgawanyiko na mipasuko ya wenyewe kwa wenyewe.
Amefahamisha kuwa kuteuliwa kwa wagombea wenye sifa na wanaokubalika watakuwa wamekirahisishia Chama cha Mapinduzi kushinda kwa kishindo ifikapo mwezi Oktoba 2025.
Amewaasa wanachama wa CCM kuacha tabia ya kuchafuana na kutengenezeana fitna kwa maslahi ya watu wachache badala yake wazidi kuungana pamoja na kushirikiana katika kukitafutia ushindi Chama cha Mapinduzi kiendelee kuongoza dola kwa miaka nitano ijayo.
Mhe. Hemed amewataka wanachama wa CCM kuendelea kudumisha Amani na Utulivu kwa kipindi chote cha maandalizi ya kuelekea uchaguzi na kuwasihi watakaoteuliwa kugombea nafasi mbali mbali wakafanye kampeni za kistaarabu zenye kuelezea mazuri yanayofanywa na viongozi wa chama na Serikali.
Amewataka wanawake na vijana wakati utakapofika kujitokeza kwa wingi katika kuchukua fomu na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Katibu wa Idara ya Siasa, Itikadi, Uwenezi na Mafunzo ya chama komred Khamis Mbeto khamis amesema wakati umefika kwa viongozi wanapotoka nje ya nchi kuelezea maendeleo yanayofanywa na viongozi wakuu wa nchi na sio kuzungumza mambo yasioku nafaida kwa Taifa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu Talib Ali Talib amesema wanachama wa CCM wa Mkoa wa Mjini wapo tayari kufanya jambo lolote lile lenye maslahi na chama na Taifa kwa ujumla.
Talib amesema Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini wamejipanga kuhakiisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 16.06.2025