SERIKALI ITAENDELEA KUIMARISHA MAZINGIRA YA UFANYAJI BIASHARA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara za huduma za kifedha ili kuvutia uwe...

Latest Post

SERIKALI ITAENDELEA KUIMARISHA MAZINGIRA YA UFANYAJI BIASHARA-MAJALIWA

Written By CCMdijitali on Thursday, July 3, 2025 | July 03, 2025


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara za huduma za kifedha ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kwa kuwa maendeleo endelevu ya taifa hayawezi kufikiwa bila ushiriki thabiti wa sekta binafsi.
 
Amesema kuwa sekta ya fedha ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa Uchumi na ustawi wa wananchi kwa ujumla na ni moja ya sababu inyowezesha maendeleo ya Taifa kwenda kwa kasi.
 
Amesema hayo leo Alhamisi (Julai 03, 2025) wakati wa uzinduzi wa Benki ya Maendeleo PLC, kuwa Benki kamili ya kibiashara, kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
 
“Endeleeni kuimarisha ushirikiano miongoni mwenu, serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya fedha katika kuchagiza maendeleo, imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia bunifu”.
 
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za kifedha zikiwemo benki kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kuelewa, kutumia na kunufaika na huduma za kifedha kwa maendeleo yao binafsi na kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.
 
“Tukifanya haya tutapunguza wizi, upotevu wa fedha kiholela kwa sababu kila mmoja atakuwa anaweza kujua fedha yake ataipataje, ataihifadhi wapi na namna ya kutoa lakini pia wapeni wateja wenu namna ya utunzaji wa fedha”
 
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Finscope huduma jumuishi za fedha zimeweza kukua kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 76 mwaka 2023. “kwa mujibu wa utafiti huo, matumizi ya huduma za benki yameongezeka na kufikia asilimia 22 mwaka 2023 kutoka asilimia 17 mwaka 2017”.
 
Kadhalika, Mheshimiwa ametoa wito kwa taasisi zote za fedha zijenge mifumo rahisi na rafiki kwa makundi yote ya watumiaji wa huduma za kifedha.
 
Awali, Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa, Muwakilishi wa Askofu Dean Chadiel Lwiza ameishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuisimamia benki hiyo na kuwa mfano wa benki iliyoanzishwa na wazawa kwa mtaji mdogo hadi kufikia kuwa benki kitaifa. “Tunaiomba benki kuu jicho lenu liwe kali kuliko letu, itazameni hii benki”
 
Kadhalika, ameongeza kuwa sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji katika biashara na usimamizi mzuri za biashara. “Tunaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoomgizwa na Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuweka mazingira haya mazuri ya ufanyaji biashara”
 
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank PLC Lomnyaki Saitabau amesema kuwa benki hiyo imejiweka katika nafasi bora zaidi ya kuwa benki ya kisasa, shindani na jumuishi kwa Watanzania wote hasa kipindi dunia inapoelekea kwenye zama mpya zenye msukumo wa kiteknolojia, ubunifu, na uwajibikaji wa hali ya juu.
 
“Kwa kufanya hivyo, tunaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassani, yenye dhamira ya kuwafikia watanzania wengi zaidi nchi nzima kupitia dira ya taifa ya ujumuishaji wa kifedha (financial inclusion) na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta binafsi, tutaendelea kushirikiana na Serikali, katika ujenzi wa Uchumi wa nchi”.
 
Naye, Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande ameipongeza benki hiyo kwa hatua kuwa iliyofikiwa na benki hiyo katika utoaji huduma kwa watanzania hasa kwa kutumia fursa zilizowekwa na Serikali “Sisi Wizara ya Fedha tumeendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki ya ufanyaji wa shughuli za kifedha, sasa wekeni mkakati wa kuifikisha benki hii maeneo mengi zaidi”.

Published from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android App

TANZANIA INAITAMBUA UHISPANIA KAMA MSHIRIKA MUHIMU - DKT MPANGO



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya wafanyabiashara wa Uhispania kwa kuwa Tanzania na Uhispania zinaweza kuunda ushirikiano wa kiuchumi wenye nguvu ili kuimarisha diplomasia ya kiuchumi.
 
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Jukwaa la Biashara la Tanzania na Wafanyabiashara wa Uhispania lililofanyika Jijini Sevilla nchini Uhispania leo tarehe 02 Julai 2025. Amesema Tanzania bado inaitambua Uhispania kama mshirika muhimu katika sekta za kimkakati kama vile nishati mbadala, miundombinu, teknolojia ya kilimo, utalii, viwanda vya rasilimali za baharini na biashara.
 
Makamu wa Rais amesema Tanzania inatambua sekta ya binafsi kama mshirika mkuu katika juhudi za maendeleo inayoongoza katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Amewakaribisha wawekezaji hao kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali zilizopo.
 
Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba Tanzania ni Taifa lenye utulivu wa kisiasa, eneo la kimkakati la kijiografia, maliasili nyingi, idadi kubwa ya vijana pamoja na uchumi unaokua kwa kasi. Ameeleza utekelezaji wa mageuzi unaofanywa na serikali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kutambua nafasi muhimu ya sekta binafsi katika maendeleo endelevu.
 
Makamu wa Rais amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Serikali imeimarisha mifumo ya sheria, miundombinu ya kisasa na kuweka dhamira thabiti ya uwazi na utawala bora. Ameongeza kwamba kwa sasa Tanzania ni kivutio cha uwekezaji katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika huku ikitoa fursa katika sekta muhimu kama vile biashara ya kilimo, utalii, nishati, madini, viwanda, uchumi wa bluu, na miundombinu.
 
Makamu wa Rais amewakaribisha kuwekeza katika maeneo ya kimkakati ikiwemo teknolojia ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni. Amesema eneo lingine la uwekezaji ni uvunaji wa rasilimali za uchumi wa bluu katika Bahari ya Hindi pamoja na Maziwa Makuu.
 
Ametaja maeneo mengine ni pamoja na uvuvi na usindikaji, uchunguzi wa madini, utalii wa pwani na baharini, usafirishaji pamoja na uwekezaji katika kuendeleza maeneo ya pwani ya Tanzania na visiwa ili kunufaika na rasilimali za uchumi wa bluu na uhifadhi wa mazingira.
 
Katika Mkutano huo Viongozi wa Sekta ya Uwekezaji wamewasilisha maeneo mbalimbali ya kuwekeza nchini Tanzania pamoja na kuonesha mageuzi mbalimbali yaliyofanyika nchini ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Pia wameeleza fursa za uwepo wa soko la uhakika wa bidhaa kutokana idadi ya watu, eneo la kijiographia la Tanzania ambalo linahudumia nchi mbalimbali, uboreshaji wa miundombinu ya msingi pamoja na maendeleo makubwa katika sekta ya TEHAMA.
 
 
Jumla ya Makampuni 31 yameshiriki katika Mkutano huo ambayo yamejikita katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo chakula na kilimo, ujenzi wa miundombinu, viwanda, sekta maji, sekta ya madini, nishati, TEHAMA, utalii pamoja na sekta ya fedha.
 
Mkutano huo umehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Aboud Mwinyi, Balozi wa Tanzania nchini Hispania mwenye Makazi yake nchini Ufaransa Mhe. Ali Mwadini, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) Gilead Teri, Meneja wa Uwekezaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Omary Omary, Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binafsi Raphael Maganga, Katibu wa Baraza la Biashara Tanzania Dr. Godwill Wanga pamoja na Kamishna wa Fedha za Nje Wizara ya Fedha Rished Bade.
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
02 Julai 2025
Sevilla – Uhispania.

Published from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android AppPublished from Blogger Prime Android App
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link