Baadhi ya Wajumbne wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Wafanyakazi Wastaafu Pemba akifutilia Hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati akiizindua rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiizindua
rasmi Bodi ya wadhamini ya Jumuiya ya Wafanyakazi Wastaafu Pemba hapo ukumbi wa
Tasaf uliopo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Chake chake Pemba.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Wastaafu wa Taasisi za Umma za Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania na zile za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
wanapaswa kushirikiana kwa karibu katika
kutumia ujuzi na Taaluma zao za muda mrefu ndani ya Jumuiya wanaazozianzisha
baada ya kustaafu kwao ili waendelee
kuchangia Maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi wakati akiizindua rasmi Bodi ya wadhamini ya Jumuiya ya
Wastaafu Pemba hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Tasaf uliopo katika Majengo ya Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar yaliyopo Chake chake Pemba.
Balozi Seif alisema mashirikiano hayo yatatoa nafasi nzuri
kwa wastaafu hao kuondoa shaka ya kuendeleza maisha yao kwani baadhi yao hupata
wakati mgumu kabla na baada ya kustaafu
kwa vile wanakuwa bado hawajajipanga.
Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi za
Umma na hata zile binafsi ambao wanaogopa kustaafu wakati utaratibu wa kufanya
hivyo upo wazi na sahihi kutokana na muongozo wa Utumishi Serikalini.
“ Tabia hii ya kuogopa kustaafu mara nyingi huwapa wakati
mgumu wafanyakazi wanaofikia umri wa kustaafu na baadhi yao bado hawajajipanga
“. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliipongeza Jumuiya ya Wastaafu Kisiwani
Pemba kwa kuanzisha Bodi ya Wadhamini ambayo itakuwa kiungo muhimu cha uhimili
wa Jumuiya hiyo.
Aliwakumbusha wanachama wa Jumuiya hiyo waendelee
kushikamana na kuvumiliana wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika njia ya
uadilivu, umoja na upendo.
Balozi Seif alieleza kwamba hatua hiyo itasaidia kuondosha
dhana potofu zinazoweza kujengwa na baadhi ya wanachama kusingizia uendeshaji
mbovu wa Jumuiya katika misingi ya ubaguzi au ubinafsi.
Akitoa Taarifa fupi Katibu wa Jumuiya ya Wastaafu Pemba
Bwana Majid Moh’d alisema Jumuiya hiyo
iliyoanzishwa mwishoni mwa mwezi wa Mei mwaka 2012 imelenga kuwataka wastaafu wafanye kazi
badala ya kubweteka na kuanza tabia ya kuomba omba ambayo haipendezi katika
Jamii.
Bwana Majid alisema wana jumuiya ya wastaafu Pemba wamepata
faraja kutokana na uongozi imara wa Bodi
ya Wadhamini wa Jumuiya hiyo ambao umeonyesha uoni mpana wa kufikiria kubuni
mipango na miradi ya kuiendeleza Jumuiya hiyo.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Katiba na Utawala Bora Pemba
Nd. Omar Khamis Juma alisema Jumuiya ya Wafanyakazi Wastaafu Pemba inafanya kazi kwa umakini
kubwa na Wizara hiyo tokea kuasisiwa kwake mwaka uliopita.
Nd. Omar alisema Taasisi hiyo wa wastaafu imekuwa ikitoa
msisimko mkubwa kwa wanajumiya wenyewe
katika kuendeleza maisha yao wakijaribu kubuni miradi tofauti ya
kiuchumi itakayooongeza mapato ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Jumuiya ya Wafanyakazi wastaafu Kisiwani Pemba imeanzishwa
Tarehe 23 Mei mwaka 2012 na kusajiliwa rasmi
mwezi Disemba mwaka 2012.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
7/1/2015.