NA BASHIR NKOROMO
HALI inazidi kuwa mbaya ndani ya Kambi ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) kufuatia taarifa za mgogoro mkubwa uliopo kati ya Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi James Mbatia.
Chanzo cha mgogoro huo ambao unafukuta, ni madai ya Slaa ya
kutomwamini Mbatia anayedai ni pandikizi anayetumiwa na serikali na Chama cha
Mapinduzi (CCM) kuvuruga umoja huo.
Inaelezwa, Slaa anamshutumu Mbatia kuwa ni Afisa wa Idara ya
Usalama wa Taifa, hivyo ni hatari kwa ustawi wa umoja huo, na kuna uwezekano
akasababisha kusambaratika kwake iwapo ataendelea kuwepo.
Chanzo hicho kilisema, msimamo huo wa Slaa umewapa wakati
mgumu vongozi wengine wa kambi hiyo na wanaona wakimtosa Mbatia watasababisha
mgawanyiko wa wanachama, hivyo kuna uwezekano mkubwa wakampuuza Katibu Mkuu
huyo.
Aidha, mbunge mmoja wa CUF akizungumza na mwandishi wa
habari hizi alisema, baadhi ya wanachama wa UKAWA wanamshutumu Mbatia kuwa
mmoja wa walioshinikiza kambi hiyo kususia mchakato wa Katiba mpya na
kushawishi wasirudi bungeni.
"Kuna mambo yanatia mashaka sana na leo viongozi wetu
wanajuta, uamuzi wa kususia bunge la Katiba haukuwa sahihi, vongozi wetu
walipotoshwa kususia bunge. Naamini kama tungebakia bungeni na kushindana kwa
hoja, kingeeleweka"
Mbunge huyo alisema, hali hiyo inaonyesha wazi kuna watu
ndani ya kambi hiyo wanatumika na CCM, na mbinu ya kushawishi UKAWA wasirudi
bungeni ilikuwa ni maagizo maalum yenye lengo la kuwapa nafasi CCM kupitisha
mambo waliyotaka kwenye Katiba mpya.
Taarifa zaidi zinasema, jambo jingine ambalo linampotezea
imani Mbatia kwa baadhi ya viongozi wenzake, ni uhusiano wake na kigogo mmoja
mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ingawa mwenyewe mara kadhaa
amekuwa akikana madai hayo na kushusha lawama kwa CCM kuhusika kusambaza madai
hayo.
Inaelezwa, Mbatia amekuwa karibu na kigogo huyo na wamekuwa
wakikutana mara kwa mara nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kupeana maelekezo ambayo hawana shaka yanalenga kufanya
hujuma kwa kambi hiyo.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na mwandishi
wa habari hizi wamesema, kambi ya UKAWA ipo kwenye wakati mgumu ukiachilia
mbali mgawanyiko uliopo katika suala la kuteua mgombea Urais kwenye uchaguzi
mkuu ujao, kuna hali ya kutoaminiana na kila mmoja anamuona mwenzake ni
msaliti.
Mchambuzi huyo aliongeza kuwa, kila mmoja ndani ya kambi
hiyo ameungana na mwenzake kwa malengo binafsi, ila hakuna mwenye imani na
mwenzake.