Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif akiwa pamoja na Viongozi wa Kitaifa na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi wakiangalia hatua za matayarisho ya mwisho ya Gwaride litakalopamba kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Brigedia Nyuki Zanzibar Brigedia General Muhaiti na kushoto yake Balozi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d na Katibu Mkuu Kiongozi Dr. Abdulhamid Yahya Mzee.
Vijana wa Muziki wa Kikazi Kipya Zanzibar wakiimba wimbo maalum utakaoburudisha kwenye sherehe za maadhimisho ya Kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12 Uwanja wa Amani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na maadhimisho ya Kitaifa
Balozi Seif akizungumza na wajumbe wa Kamati hiyo walipokuwa wakitathmini
matayarisho ya kwisho ya kilele cha sherehe za Mapinduzi zinazofikia ukingoni
Januari 12 2015 uwanjani Aamani.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Matayarisho ya mwisho kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya
kusherehekea kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yamefikia
hatua ya mafanikio makubwa katika
kukamilika kwake.
Maadhimisho hayo yaliyoanza Tarehe Pili Januari 2015 kwa usafi wa mazingira,
uzinduzi pamoja na uwekaji wa mawe ya
msingi ya miradi mbali mbali ya Taasisi za Umma na zile binafsi yakiwemo
mashindano ya michezo na burdani tofauti yanafikia kilele chake Januari 12 siku
ambayo wakwezi na Wakulima walijikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni.
Vikosi vya ulinzi na usalama vya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania na vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vilikamilisha matayarisho
ya mwisho ya Gwaride rasmi hapo Uwanja
wa Amani Mjini Zanzibar linalotarajiwa kupamba maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa
ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akiambatana na baadhi ya Viongozi wa Kamati 10 zilizopewa jukumu la kusimamia
maandalizi ya sherehe hizo walishuhudia gwaride la vikosi hivyo vinavyoonekana
kuwiva katika kiwango kilichokusudiwa.
Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ }, Polisi,
Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo { KMKM }, Mafunzo,Jeshi la Kujenga Uchimi {
JKU }, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi na Valantia vilionekana kuupamba uwanja wa
amani kwenye matayarisho hayo vikiwa tayari kwa ajili ya Kilele cha maadhimisho
hayo.
Gwaride hilo lililoongozwa na Luteni Kanali Moh’d Khamis
Adam liliambatanisha pia na matayarisho mengine ya mwisho ya ngoma za utaduni
pamoja na muziki wa Kizazi kipya watakaopata fursa ya kutoa burdani kwenye
kilele cha maadhimisho hayo ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho
ya Kitaifa katika Ukumbi wa Watu mashuhuri { VIP } uliopo Uwanja wa Amani Mjini
Zanzibar mara baada ya kuangalia
matayarisho hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi Seif aliyapongeza
majeshi yote kwa hatua yaliyochukuwa ya kushiriki vyema kwenye maandalizi ya
sherehe hizo.
Balozi Seif alisema juhudi zilizoonyeshwa na wapiganaji hao
katika kulichapa gwaride zimeonyesha
wazi umahiri wao katika kutekeleza vyema majukumu wanayopangia na Taifa.
“ Nimeridhika na maandlizi yote yaliyochukuliwa na Kamati zote zilizoshiriki kikamilifu katika matukio mbali mbali tokea sherehe zetu zilipoanza Mapema mwezi huu. Mambo mazuri sana licha ya kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza ambazo uwezo wa kuzikamilisha upo “. Alisema Balozi Seif.
Mapema Katibu wa Kamati ya Sherehe na Maadshimisho ya
Kitaifa Dr. Khalid Salum Moh’d alisema
Kamati imeandaa utaratibu kwa Wananchi watakaokosa kuingia ndani ya Uwanja wa Amani kuziona sherehe hizo kupitia TV
maalum zitakazowekwa upande wa jukwa la mashariki { Maarufu jukwaa la Urusi }.
Dr. Khalid alisema TV hizo zimeandaliwa kwa lengo la
kupunguza msongamano mkubwa unaoweza kutokea endapo wananchi watajitokeza kwa
wingi kuhudhuria sherehe hizo za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 51.
Wageni wa Kimataifa wapatao 120 miongoni mwao
wakiwemo Mabalozi 80 wa Nchi za
Nje waliopo Tanzania wamethibitisha kuhudhuria sherehe hizo, waandishi wa
Habari 160 wataripoti matukio ya sherehe
hizo wakati vituo vya TV Vinne na Redio 6 vinatarajiwa kutangaza moja kwa moja
sherehe hiyo.