Home » » MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AHUDHURIA SHEREHE ZA MAULIDI YALIYOANDALIWA NA JUMUIYA YA SUNNI MUSLIM JAMAT JIJINI DAR ES SALAAM.

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AHUDHURIA SHEREHE ZA MAULIDI YALIYOANDALIWA NA JUMUIYA YA SUNNI MUSLIM JAMAT JIJINI DAR ES SALAAM.

Written By CCMdijitali on Monday, January 5, 2015 | January 05, 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam kulia yake Al-Hajj Mussa Salum na Mbunge wa Mpendae Mh. Salum Turky Kushoto yake  walipokuwa kwenye kisimamo cha kiyamu wakati wa  kumsalia Mtume Muhammad {SAW } kwenye sherehe za maulidi yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Sunni Muslim Jamat Jijini Dar es salaam.
 Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Jumuiya ya Sunni Muslim Jamat wakisimama kumsalia Mtume Muhammad { SAW } HAPO Kitumbini Jijini Dar es salaam.
 Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam Ah – Hajj Mussa Salum akiipongeza Jumuiya ya Sunni Muslim Jamat ya Mtaa wa Kitumbini Dar es salaam kwa kuhimili majaribu mbali mbali iliyopata tokea ilipoanzishwa.
 Balozi Seif akizungumza katika hafla ya maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad {SAW } yaliyofanyika katika Msikiti wa Jumuiya Sunni Muslim Jamati Mjini Dar es salaam.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam Al –Hajj Mussa Salim wanzo kushoto akimpongeza Balozi Seif baada ya kuvishwa Mkashda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Sunni Muslim Jamati Sheikh Abdullhamid Abdulkarim aliyepo kulia mwisho mwa maulidi ya Jumuiya hiyo Mjini Dar es salaam.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.


Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwambna Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini wanapaswa na wajibu wa kuisoma Historia ya Kiongozi wa Dini hii Mtume Muhammad { SAW } ili vijana na jamii yote kwa jumla ielewe kiundani utukufu na ubora wa Dini ya Kiislamu.

Alisema hatua hii itatoa fursa kwa wasomi hao kuzijua changamoto na mafanikio yanayotokana na uongozi uliotukuka wa Mtume Muhammad { SAW } ambao ni mfano tosha wa kuigwa kwa waumini pamoja na viongozi wa kada zote.

Balozi Seif alisema hayo wakati wa sherehe ya maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad { SAW } yalioyoandaliwa na Baraza la wadhamini wa Jumuiya ya Sunni Muslim Jamaat iliyopo Mtaa wa Mosque, Kitumbini Jijini Dar es salaam.

Alisema licha ya kuenea kwa vugu vugu la Dini ya Kiislamu katika pembe zote za Dunia lakini moyo wa kujitolea kwa baadhi ya waumini katika harakati za kusimamisha Dini unaonekana kupungua kasi.

Balozi Seif alieleza kuwa jamii imekuwa ikishuhudia madrasa nyingi nchini zikikosa walimu wa kujitolea katika kusomesha vijana wenzao kwa dhana ya kudai maslahi yao kwanza  badala ya kuangalia akhera yao.

Alisema ni wajibu wa kila Muumini kuhakikisha kwamba dini ya kiislamu inasimama kwa hali yoyote ile ili kuunga mkono kazi kubwa aliyoifanya Kiongozi huyo ambayo alipewa na mola mtukufu kuitekeleza.

Balozi Seifahamisha kwamba Mtume Muhammad alianza harakati za kusimamisha dini ya Kiislamu mara tu alipopewa utume akiwa na umri wa miaka 40 na kuifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 23.

Hata hivyo Balozi Seif alisema Kioingozi huyo alikumbwa na changamoto nyingi akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na kufanyiwa lugha za kejeli, vitendo vya maudhi pamoja na mapigano kati ya wale waliomfuata na wale waliomkanusha.

“ Mapigano kati ya wale waliomfuata na wale waliomkanusha lakini pia Mtume Muhammad alipata mafanikio makubwa  sana ambayo kila mmoja wetu anatakiwa ajitahidi alau ayakaribie mafanikio hayo kubwa zaidi subra na uvumilivu “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisisitiza kwamba kazi kubwa inayowakabili waislamu katika maisha yao kwa sasa ni kuhakikisha Historia ya uzawa, malezi na uongozi wa Mtume katika kusimamisha dini ya Kiislamu inaimarishwa ili wafanikiwe katika maisha yao ya dunia na yale ya milele.

Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa  Jumuiya ya Sunni Muslim Jamaat iliyopo Mtaa wa Mosque, Kitumbini Jijini Dar es salaam kwa jitihada zake za kuandaa hafla hiyo ya kheir ambayo itaendelea kuwa kielelezo kwa jamii ya Kiislamu hapa Nchini.


Mapema Mjumbe wa Baraza la wadhamini wa Jumuiya ya Sunni Muslim Jamat Sheikh Said Abdull – Haji alisema Baraza hilo liko katika matayarisho ya mwisho ya kuunda Kamati ya Baraza.

Sheikh Said alisema kamati hiyo itapatikana baada ya wana Jumuiya hiyo kuwachaguwa Viongozi watakaounda Kamati hiyo na kuifanya Jumuiya kukamilisha Uongozi wake kufuatia misuko suko iliyoipata kwa takriban miaka 21 iliyopita.

Alifahamisha kwamba Sunni Muslim Jamat imejiwekea malengo ya muda mrefu katika uanzishaji wa  taasisi za Elimu, ujenzi wa nyumba za Makaazi, huduma za afya ili kuijengea uwezo Jumuiya hiyo iliyoasisiwa kwenye kitovu cha msikiti wao tokea mwaka 1907.

Naye Imamu Mkuu wa Msikiti wa Sunni Muslim Jamat Maulana Faiz aliwakumbusha waumini wa Dini ya kiislamu kuendelea kushikamana vitendo vilivyopewa nafasi ya juu na Masahaba waliyosimamia Dini ya Kiislamu.

Maulana Faiz alisema uislamu ni Dini kamili iliyokamilika muundo wake inayompa uwezo na fursa mwanaadamu kuendesha harakati zake za kimaisha katika misingi ya amani na uungwana.

Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuwawaa-idhi waumini hao Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam Al – Hajj Mussa Salum alisema yapo matumaini makubwa kwa jumuiya ya Sunni Muslim Jamat ya ya kusaidia kuendeleza Dini  na fikra za waumini wa Dini ya Kiislamu.

Al – Hajj Mussa Salum alisema Jumuiya hiyo imepita katika majaribu makubwa ambayo kwa kiasi Fulani yamechangia kupunguza kasi ya malengo ya Taasisi hiyo ya Kidini.

Katika hafla hiyo ya kusherehekea uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } iliyoandaliwa na Jumuiya ya Sunni Muslim Jamat Makamu wa Pili mwa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi tuzo na vyeti kwa waasisi mbali mbali waliochangia kuendeleza Jumuiya hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/1/2014.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link