Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiiifungua rasmi Skuli ya Sekondari ya Rajaja iliyopo Kwamtipura Wilaya ya Mjini Mkoa wa Majini Magharibi. Zanzibar.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Faraja Mwalimu Ameir Khamis Bakar aliyevaa suti nyeusi akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kuizindua rasmi Skuli hiyo.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Mh. Ali Juma Shamuhuna na nyuma ya mwalimu Mkuu Ameir ni Mkuu wa Wilaya ya
Mjini Kanal Mstaafu Abdi Mahmoud Mzee.
Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekomndari ya Faraja wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri wakati wa hafla ya ufunguzi wa skuli yao uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Baadhi ya walimu wa Skuli ya Sekondari ya Faraja wakiwa
makini katika kusikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa Skuli yao Balozi
Seif ambae hayupo pichani.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema kwamba hakuna hakiba, utajiri au urithi wenye thamani kubwa ambao mzazi
anaweza kumuachia mtoto wake isipokuwa elimu.
Alisema ukweli ni kwamba mtoto akipata elimu tayari anakuwa
na rasilmali ya maisha yake yote ambayo ndio inayompa utajiri wa kudumu
usioweza kuibiwa au kuharibiwa.
Balozi Seif alisema hayo wakati akiifungua rasmi Skuli ya
Sekondari ya Faraja iliyopo katika mtaa wa Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni
miongoni mwa shamra shamra za kusherehekea maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema wazazi wana wajibu wa kushirikiana na walimu na
kamati za skuli katika kuwahimiza watoto kwenda kutafuta elimu ili kuungana na
Serikali katika dhana nzima ya kuwajengea mazingira mazuri ya miundo mbinu ya
kielimu watoto wote hapa nchini.
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali itaendelea kuchukuwa
hatua mbali mbali katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa skuli na huduma nyengine
muhimu za Kijamii zinapelekwa katika na maeneo wanayoishi wananchi
waliowengi wengi ili kuwapunguzia
usumbufu wa kufuata huduma hizo masafa marefu.
Alisema Taifa limeamua kuwekeza katika sekta ya elimu
ikielewa kwamba nchi itapiga hatua kubwa
za maendeleo iwapo wananchi wake wataelimika. Hivyo aliwaasa wanafunzi kutumia fursa walizozipata ili baadaye waweze
kulitumikia Taifa lao katika nafasi tofauti za kitaalamu na hata za uongozi.
“Kujengwa kwa Skuli hii hapa kumelengwa kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wa kufuata skuli maeneo mengine ya mbali “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba jamii
imekuwa ikishuhudia juhudi kubwa za Serikali ilizochukuwa katika kujenga Skuli
za Sekondari 19 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ikiwa inatekeleza
Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
Alisema Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Mheshimiwa
Dr. Ali Mohammed Shein tokea kuingia madarakani miwaka mine iliyopita imeamua
kuongeza uwekezaji katika upanuzi wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu
ya sekondari na vyuo Vikuu.
Balozi Seif alisema kwamba Serikali imeamuwa kufanya hivyo
ikilenga kutekeleza kwa vitendo maamuzi yaliyofikiwa tokea mwaka 1964 chini ya Rais wa Kwanza wa
ZXanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kutoa elimu bila ya malipo kwa
watoto wote bila ya ubaguzi.
Alifahamisha kwamba lipo ongezeko la wanafunzi kutokana na
juhudi hizo ambapo takwimu zikionyesha kwamba mwaka 2010 kulikuwa na wanafunzi
346,377 katika ngazi zote za elimu hapa Zanzibar ikilinganishwa na mwaka 2014
uliobeba jumla ya wanafunzi Laki 388,719.
Alisema takwimu hizi zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la
wanafunzi katika kipindi hicho cha miaka
minne ikiwa ni kielelezo cha wazi cha nia ya Serikali katika kuimarisha sekta
ya elimu na kuweza kupambana na umaskini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwanasihi
wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya skuli za Umma pamoja na wanafunzi wanaoitumia skuli
hizo hawana budi kuzitunza vyema ili ziendelee kutoa huduma kwa muda mrefu
zaidi.
Alisema Serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa
miundombinu ya ujenzi wa skuli mbali mbali, hivyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali inapaswa kuandaa utaratibu maalum wa utunzaji wa majengo ya skuli ili
kuhakikisha yanaendelea kuwa katika hali nzuri kila wakati.
Akisoma Risala ya Walimu na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari
ya Faraja Mwalimu Takadiri Omar Bakar
alisema skuli hiyo iliyojengwa kwa Mkopo wa Benki ya Dunia ilianza na wanafunzi
838 mwaka 2013.
Mwalimu Takadir alisema hivi sasa skuli hiyo yenye walimu 71
imeongeza idadi ya wanafunzi wanaofikia 1674 na kuifanya kuwa na upungufu wa
walimu wa masomo ya Sayansi.
Alisema ujenzi wa skuli hiyo umesaidia kupunguza ongezeko
kubwa la wanafunzi katika skuli za Rahaleo na Muembe Ladu pamoja na
kuwaondoshea usumbufu wa masafa marefu wanafunzi wa maeneo ya Ng’ambo.
Hata hivyo Mwalimu Takadiri alielezea changamoto
zinazoikabili skuli ya Faraja akazitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na ukosefu
wa huduma za maji safi, uhaba wa compyuta pamoja na walimu wa sayansi kutokana
na idadi kubwa ya wanafunzi pamoja na ukosefu wa uzio unaoizunguuka skuli hiyo.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar Bibi Khadija Saleh alisema
Skuli ya Faraja iliyojengwa Kwa Mkopo wa Benki ya Dunia wa gharama ya Shilingi
Bilioni 1.8 ina mazingira rafiki ya wanafunzi wote wakiwemo watoto wale wenye
mahitaji Maalum.
Bibi Khadija alisema katika kuijengea mazingira mazuri ya
utoaji wa elimu inayokwenda na wakati Skuli hiyo ya Faraja Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar itajitahidi
kuzichukulia hatua inayofaa changamoto zote
zinazoikabili skuli hiyo ambazo zimo ndani ya uwezo wa Wizara hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/1/2015.