Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mabomba ya kusambazia maji
safi Diwani ya Wadi ya Upenja Bibi Asha Abdulla Mussa kwa ya Kijiji cha
kilombero Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kati kati yao ni Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleiman Iddi.
Mabomba ya kusambazia maji safi katika Kijiji cha Kilombero yenye gharama ya shilingi Milioni 17,000,000/- yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitopo Balozi Seif Ali Iddi.
Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akishiriki katika kazi ya uchimbaji mtaro kwa ajili ya ulazaji wa mabomba kwa ajili ya huduma za kusambazia maji safi
katika Kijiji cha Kilombero.
Picha na Hassan Issa wa – OPMR – ZNZ.
Press Release:-
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema licha
ya juhudi zinazochukuliwa na viongozi katika kuchangia nguvu za kukabiliana na
matatizo mbali mbali yanayowakabili wananchi katika maeneo yao lakini bado
jukumu hilo litaendelea kubakia mikononi mwa
wananchi wenyewe.
Alisema Viongozi na hata Serikali Kuu huhamasika na kushawishika zaidi kusaidia hata
uwezeshaji na hata vifaa kwenye miradi
ya Jamii baada ya kuona nguvu za Wananchi zimeanza au kuiendelezwa katika
kujikomboa na umaskini au kujitafutia
maendeleo yao.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alisema hayo wakati akikabidhi mabomba 250 ya kusambazia huduma za
maji safi na salama kwa ajili ya Wananchi wa Kijiji cha Kilombero hapo
katika kituo cha Kilimo Kilombero Wilaya
ya Kaskazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mabomba hayo yaliyogharimu jumla ya shilingi Milioni
17,000,000/- nusu ya gharama ya fedha hizo imetokana na mfuko wa Jimbo { CDF }
na nusu iliyobakia imetolewa na Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.
Balozi Seif pia alishiriki kazi ya uchimbaji mtaro wa
ulazaji wa bomba hizo unaoanzia kwenye kisima kilichochimbwa kwa ajili ya mradi
huo wa usambazaji maji ambacho kimeshakalimika uliokwenda sambamba na
upatikanaji wa huduma za umeme katika kisima hicho.
Aliwapongeza wananchi wa Kijiji cha Kilombero kwa kazi kubwa
wanayoendelea kuifanya ya kujiondoshea matatizo yanayowakabili ikiwemo
kushiriki katika kazi za usambazaji wa huduma za maji safi.
Balozi Seif alisema huduma za upatikanaji wa maji safi ni
zao hivyo lazima wahakikishe wanashiriki kwa nguvu zao zote katika kukabiliana
na changamoto kama hizo za jamii.
Aliwaeleza wananchi hao wa Kijiji cha Kilombero kwamba
jitihada zitaendelea kuchukuliwa na
Uongozi wa Jimbo hilo za kusambazwa huduma za maji safi na salama katika mitaa
ya kijiji hicho mara baada ya Bomba za maji hayo kufikishwa katika eneo la
Skuli ya Kilombero kutoka kwenye kisima hicho.
“ Suala la tataizo la huduma za maji safi ndani ya kijiji cha Kilombero litaendelea kubakia katika historia siku chache zijazo “. Alisema Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi.
Aliendelea kuwaasa wananchi hasa vijana kujiepusha na tabia
ya kushawishiwa na baadhi ya Watu wakiwemo wanasiasa katika kujiingiza kwenye
uchochezi unaozaa balaa na matatizo.
Balozi Seif alisema ni vyema kwa wananchi hao wakalazimika
kuelewa athari ya uchochezi unaofanywa na wanasiasa hao ambao mara nyingi unalenga kuwanufaisha
wao binafsi.
Mapema Diwani wa Wadi ya Upenja Bibi Asha Abdulla Mussa akipokea
mchango wa mabomba hayo ya usambazaji maji safi katika Kijiji cha
Kilombero alimpongeza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope kwa moyo wake wa kusaidia
kuondosha matatizo yanayowakabili wananchi wa Jimbo lake.
Diwani Asha alimuomba Mbunge huyo kuendelea na juhudi
hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa
zikileta faraja kwao Viongozi wa wadi na Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo hilo pamoja na wananchi wote.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha
Kilombero Msimamizi wa Kamati ya mradi
wa Maji ya Kijiji hicho Bwana Moh’d Haji Faki alimuhakikishia mbunge huyo wa
Jimbo la Kitope kwamba Wananchi wa Kijiji hicho wako tayari muda wowote
kushiriki katika kazi za maendeleo wakati watapotakiwa kufanya hivyo.
Bwana Moh’d alisema mradi huo wa usambazaji huduma za maji
safi katika Kijiji hicho ni miongoni mwa kazi hizo ambazo wataendelea
kushirikiana katika kuzitekeleza kwa faida yao na ustawi wa vizazi vyao.
Zaidi ya shilingi Milioni 20,000,000/- zilizotolewa na
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi zimetumika katika ujenzi wa Kisima cha Maji ya Kilombero kwa lengo la
kuwaondoshea usumbufu wa miaka mingi wa huduma za upatikanaji wa maji safi na
salama wananchi wa Kijiji hicho.