Home » » Watoto 18 waliofungiwa Moshi wadai kubebeshwa matofali mgongoni

Watoto 18 waliofungiwa Moshi wadai kubebeshwa matofali mgongoni

Written By CCMdijitali on Tuesday, March 10, 2015 | March 10, 2015

Baadhi ya watoto 18 waliokuwa wakihifadhiwa kwenye nyumba iliyopo Kata ya Pasua, mkoani Kilimanjaro. Picha na Dionis Nyato 

Na Rehema Matowo na Fina Lyimo,Mwananchi

Kwa ufupi
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela imeeleza kuwa hayo yalibainika katika mahojiano baina ya watoto na askari wa dawati la jinsia.


Moshi. Jeshi la Polisi wilayani hapa, limedai kuwa watoto waliokutwa ndani ya nyumba katika eneo la Pasua, Manispaa ya Moshi siyo wakazi wa Kilimanjaro na walikuwa wakiishi kwenye mateso makubwa.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela imeeleza kuwa hayo yalibainika katika mahojiano baina ya watoto na askari wa dawati la jinsia.

Alisema watoto hao wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo Tanga, Mara, Kagera, Mbeya na Dodoma.

Kamanda Kamwela alisema pia wamegundua kuwa watoto walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu ikiwamo kulala chini katika chumba kidogo.

Alisema polisi linawashikilia watu wawili (mume na mke) ambao wanatuhumiwa kuwahifadhi watoto hao.

Kamanda huyo alisema watoto hao wana umri wa kwenda shule, lakini walikuwa hawasomi.

Alisema polisi wanachunguza aina ya masomo ya dini waliyokuwa wakifundishwa.

“Lazima tuchunguze uhalali wa masomo ya dini waliyokuwa wakisoma ili tujue kama kweli watoto hawa walipelekwa na wazazi wao au la, kwa kuwa watoto hao walipaswa kuwa shuleni” alisema Kamanda Kamwela.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga alisema watoto hao walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu, huku wakipewa adhabu kali ikiwamo kubeba matofali mgongoni pindi wanapokosea.

“Maelezo ya watoto yanaonyesha walikuwa wakiteswa, adhabu hizi kwa watoto ni kubwa, bado tunawachunguza ili tujue kila kitu na walichukuliwaje huko majumbani kwao,” alisema Makunga.

Alisema kwa wazazi watakaowatambua watoto wao, wanapaswa kwenda na uthibitisho ikiwamo cheti cha kuzaliwa au uthibitisho mwingine utakaoonyesha ni mzazi halisi.

Makunga alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa, watuhumiwa hao wana kituo kingine kinachohifadhi watoto.

Alisema kwa sasa hawezi kueleza zaidi hadi polisi watakapomaliza upelelezi wao.

Majirani wanena

Aisha Mohamed na Marsela Minja ambao ni majirani wa watuhumiwa walidai kuwa awali nyumba hiyo ilikuwa na mmiliki mwingine, lakini alijinyonga miaka michache baada ya kuuza eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walidai kuwa mmiliki wa kwanza wa nyumba hiyo alikuwa na ujirani mwema na wakazi wa eneo hilo.

Marsela alisema mmiliki wa sasa tabia yake ni tofauti kwa kuwa anawazuia watu kuchota maji na pia kajenga ukuta mrefu kuzingira nyumba hiyo.

Alisema tangu mmiliki huyo ahamie katika nyumba hiyo miaka mitatu iliyopita, hawakuwa na mazoea na jirani yeyote.

Wananchi hao walidai wiki mbili zilizopita mmiliki huyo alifunga ndoa na wao walishuhudia magari mawili ya kifahari yakiingia kwenye geti na baada ya muda yaliondoka.

“Sisi hatuwafahamu sana kwa sababu hutoka na magari wakiwa wamejifunika hadi usoni, hivyo siyo rahisi kuwafahamu...hatujawahi kuwaona watoto wakienda shule wala dukani,” alisema Marsela.

“Ukipita kwa huku nyuma ndiyo utawasikia wakifundishwa masuala ya dini, lakini wakikosea wanapewa adhabu ya kupanda ukuta , lakini hata ukiwasemesha hawajibu zaidi ya kulia,” alisema Aisha.

Mtaalamu azungumza

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki alisema kitendo cha watoto hao kukosa uhuru na mazingira ya kuchangamana na watu wa aina mbalimbali kitawaathiri kisaikolojia.

“Wasiposaidiwa kuendana na mazingira hata wakitoka watakuwa na matatizo, kwa sababu walishakosa baadhi ya hatua muhimu katika makuzi yao, kwa sababu mtoto anapopelekwa shule siyo kwa ajili ya kusoma tu bali kuchangamana,” alisema Dk Mauki.

Chanzo

Sakata la watoto hao liligundulika Machi 7 mwaka huu, saa 12.00 jioni baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa mzazi mmoja mkazi wa Kata Pasua aliyedai watoto wake watatu kutoroshwa.

Mzazi huyo aliwaambia polisi kuwa alipata taarifa kuwa watoto wake wamehifadhiwa katika nyumba hiyo, ndipo askari walipofuatilia na kuwakuta watoto 18.

Juzi saa tatu asubuhi, mamia ya wakazi wa Moshi walifika katika nyumba hiyo, huku wakiimba kutaka kuwaona watoto wao baada ya kuwakuta askari kanzu wakilinda eneo hilo.

Askari hao walizidiwa nguvu na kukiita Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwenda kuwatawanya wananchi ili watoto hao watolewe na kupelekwa kituoni kwa mahojiano.

Baadaye Mkuu wa Kituo cha Polisi Moshi, Deusdedit Kasindo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Norvatus Makunga walifika katika nyumba hiyo na kuzungumza na mmiliki.

Mmiliki huyo alidai watoto hao walipelekwa na wazazi wao kwa lengo la kufundishwa dini. Polisi waliwachukua watoto hao na kuwapeleka kituoni kwa mahojiano.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link