Na Kelvin Matandiko
Dar es Salaam. Balozi Amina Salum Ali amesema Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, Dk Ali Mohamed Shein bado anastahili kupewa nafasi ya kuongoza Wazanzibari.
Balozi Amina ambaye ni Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Marekani alitoa kauli hiyo jana katika Kipindi cha Funguka’, kilichoanza kurushwa na Azam TV, baada ya kuulizwa swali na mwendeshaji wa kipindi, Tido Mhando.
Mwanadiplomasia huyo alitoa jibu hilo alipoulizwa kwa nini hakutaka kugombea tena urais wa Zanzibar wakati alionyesha nia ya kuongoza Zanzibar mwaka 2000.
Akijibu swali hilo alisema, “Kwa sasa tunapita kwenye kipindi kigumu na mie ninakiri kwamba, Rais tuliyenaye anajitahidi, kwa sababu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ni mpya, hajamaliza muda wake na tunaona jinsi alivyoongoza,” alisema.
Alisema ni vyema Dk Shein akapewa nafasi ya kuendelea kuongoza licha ya kuwapo kwa wanachama wanaotamani nafasi hiyo.
Mwombaji huyo wa urais wa muungano kupitia CCM alisema Wazanzibari wengi wameonyesha nia ya kumwamini Dk Shein.
Kuhusu SUK na hali ya kutofautiana kisiasa, Balozi Ali alisema umoja huo ulikuwa ni majaribio ambao umeonyesha unafuu mkubwa katika mahusiano ya Wazanzibari, hivyo serikali hiyo haitakiwi kuvunjwa.
Kuhusu Muungano
Akizungumzia mahusiano ya muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Balozi Ali alisema changamoto kubwa iliyopo ni kukosekana kwa utekelezaji wa mambo yanayojadiliwa ndani ya vikao vya serikali hizo mbili.“Mambo yalijadiliwa na kukubaliwa lakini kila jambo lilionekana kama ni nyeti au la kisiasa au haliwezekani, matokeo yake mambo yamekuwa ni mengi mpaka kufikia hatua ya kufanyia mapitio ya katiba,”alisema na kuongeza:
“Mambo yanayowaumiza Zanzibar ni masuala ya uchumi na upande mwingine ni masuala ya kisiasa na Itifaki. Ilikuwa wakati mwafaka wa kuyafanyia maboresho, ukiangalia katika mapendekezo ya Katiba kama kuna mambo ambayo yangefanyiwa kazi, yangeweza kuleta nafuu katika mfumo wetu,” alisema.
Alipoulizwa ni kwa jinsi gani ataondoa kero na changamoto za muungano huo, mgombea huyo alisema Muungano huo haukuwa na kero ila zilikuwa changamoto tu ambazo zimebadilika kuwa kero baada ya kuchukua muda mrefu bila kushughulikia.
Alisema; “Kwa mfano suala la Benki Kuu au ugawanaji wa mapato, pia tulikubaliana kuwa na ufumbuzi wa muda katika ugawanaji mapato, lakini kama ni hiyo pia kulikuwa na tume ya pamoja ya fedha ndani ya Katiba lakini haikuanzishwa.
“Sasa kama kuna jambo ambalo hamlimalizi leo, litakuwa kero tu..sasa mimi sijaona kero hapo ila kwa kuwa serikali zetu mbili tumeshindwa kutatua, nia ya dhati ya kuondoa kero hizo lazima ionekane kwa vitendo.
Serikali yake
Akizungumzia aina ya serikali yake atakayoitumia baada ya kupewa ridhaa na Watanzania kupitia CCM, alisema kipaumbele chake ni kufufua viwanda vya ndani ili kuongeza kipato cha Watanzania.Pia alisema rushwa, ubadhirifu, ufisadi, mikataba mibovu na kutojali wananchi ni mambo ambayo yameendelea kuwaumiza Watanzania.
Alipoulizwa juu ya mazingira ya kuogopana kwa viongozi katika kuwashughulikia mafisadi, Balozi Ali alisema utaratibu uliopo ufanyiwe marekebisho ili wahusika washughulikiwe.
Alisema ni muhimu kuweka mahakama maalumu na mtuhumiwa kusimamishwa kwa muda.
“Kesi siyo isichukue miaka sita, pia uwajibikaji siyo majadiliano, inapotokea lazima waziri awajibike mara moja, unapokuwa rais na chama chako unapewa dhamana tu na inapotokea kosa lazima uwajibike kisiasa,lakini naona imekuwa tatizo mpaka mtu aondolewe na rais, hapana.”
alisema na kuongeza:
Kuhusu hali ya kujitokeza kwa wingi wagombea urais, Amina alisema; “ Siyo tatizo ila urais si jambo la majaribio, tuwaachie Watanzania wachague mwenye sifa, aliyekuwa bora, mwenye uwezo na mimi ninazo sifa zote na ninaamini kuwa bora zaidi kuliko wote.”
Chanzo: Mwananchi