Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijuika pamoja na Watumishi na Wananchi wa Wilaya ya Magharibi”B” katika usafi wa mazingira kwenye mtaro wa maji ya Mvua uliopo Kwa Kira karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kusherehekea maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika Tarehe 9 Disemba.
Wa Pili kutoka Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dr. Mwinyihaji Makame akiwa miongoni mwa Watumishi wa Umma waliojitokeza kushiriki usafi wa mazingira kuadhmisha siku ya Uhuru wa Tanganyika hapo Kwa kira.
Wa Kwanza kutoka Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Nd. Ayoub Mohammed Mahomud na mwenye pauro aliyeinama kwenye Mtaro ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Watanzania Nchini kote leo wameungana pamoja katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Jamuhuri ya Tanganyika iliyojikomboa kutoka katika Utawala wa Kingereza Tarehe 9 Disemba Mwaka 1961ambapo imeshafikia miaka 54 sasa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dr. John Pombe Joseph Magufuli aliagiza mwaka huu Watanzania washerehekee kwa usafi wa mazingira ili kupunguza au kuondoa kabisa ugonjwa wa Kipindu Pindu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliungana na Watumishi pamoja na Wananchi wa Wilaya ya Magharibi “B” katika usafi wa mazingira kwenye eneo la mtaro wa maji ya Mvua uliopo kwa Kira karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kuelekea Kiembe Samaki.
Sherehe za mwaka huu zimeadhimishwa kwa staili ya aina yake kwa Watendaji na Wananchi kufanya kazi za Kujitolea katika kusafisha mazingira kwenye maeneo na Ofisi zao kuitikia Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Abdulhamid Yahya Mzee ya kuwaagiza watumishi wote wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuripoti makazini mwao
kama kawaida.
Zoezi hilo la usafi wa mazingira lilikuwa na lengo maalum la kuwapa fursa Wazanzibari kuungana na wenzao wa Tanzania Bara katika maadhimisho hayo ya Uhuru wa Jamuhuri ya Tanganyika
Tarehe 9 Disemba ya kila mwaka.
Akizungumza na washiriki wa zoezi hilo la Usafi wa mazingira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema umefika wakati kwa Jamii lazima ibadilike katika kudumisha usafi wa mazingira kwa lengo la kujiepusha na miripuko ya maradhi mbali mbali.
Balozi Seif alisema ni vyema ukaandaliwa utaratibu maalum wa kuwapa fursa Wananchi wote kutenga siku Moja ya kila mwezi washiriki kazi za usafi wa mazingira katika maeneo yote wanayoishi.
“ Itokee siku moja ndani ya kila mwezi kutenga muda kwa kufanya usafi wa mazingira na hata kufunga Maduka na biashara nyengine zikasita kwa muda ili kutoa muda japo mdogo wa kushiriki zoezi hilo muhimu “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliasa kwamba tabia ya kukosa nidhamu kwa baadhi ya watu mitaani na hata sehemu za kazi kwa kutupa taka taka ovyo haipendezi na kwa kweli inarejesha nyuma ustawi wa Jamii.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Magaribi “B” Nd. Ayoub Mo’hd Mahmoud ameupongeza Uongozi wa Mfuko wa Bara bara Zanzibar kwa jitihada zake inazochukuwa katika kusaidia vifaa kwa ajili ya shughuli za Usafi wa Mazingira kwenye Wilaya hiyo.
Nd. Ayoub alisema Uongozi huo wa Mfuko wa Bara bara pamoja na Watendaji wake umekuwa ukitoa ushirikiano mkubwa kwa Ofisi yake kiasi kwamba ipo haja kwa Taasisi nyengine kuiga mfano huo bora.
“ Tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na Uongozi wa Mfuko wa Bara bara katika kuimarisha usafi pamoja na utengenezaji wa Bara bara zilizomo ndani ya Wilaya yetu “.
Alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya ya Magharibi “B”.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara Zanzibar { UUB } Mhandisi Shomari Ali Shomari alisema mpango maalum umeandaliwa na Idara hiyo katika kuona Bara bara itokayo Uwanja wa Ndege hadi Mjini inakuwa katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.
Alisema Bara bara hiyo muhimu ni kielelezo na haiba ya Mji wa Zanzibar inayotoa sura halisi kwa wageni na watalii wanaoamua kufunga safari ya kuitembelea Zanzibar.
Mhandisi Shomari alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa makusudi ili kulinda na kuhifadhi sifa halisi ya Zanzibar katika ukarimu wake wa Kihistoria kwa wageni wanaoitembelea.
Usafi wa mazingira pia ukaonekana kushamiri ndani ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar ambapo watendaji wa Ofisi hiyo walijumuika pamoja katika kusafisha sehemu mbali mbali za Jengo hilo.
Kazi hizo iliyoanza mapema asubuhi ilijumuisha watendaji wa ngazi zote wakiongozwa na wakurungezi wa Idara zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/12/2015.