Home » » Balozi Seif ahutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani

Balozi Seif ahutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani

Written By CCMdijitali on Monday, April 25, 2016 | April 25, 2016

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiyaongoza Matembezi ya maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyoanzia mbele ya Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Mazizini na Kuishia viwanja vya Maisara Suleiman.

Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo na Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Juma Malik Akil.

 Baadhi ya vikundi vya mazoezi Nchini zikishiriki kwenye matembezi ya maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani zilizofikia kilele chake uwanja wa Maisra Suleiman Mjini Zanzibar.
 Wanavikundi vya mazoezi ya viungo wakinyoosha miili yao mara baada ya kumaliza matembezi yao kuadhimisha siku ya Malaria Dunani yanayofanyika kila ifikapo Tarehe 25 ya Mwezi April.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akihutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani zilizofikia kilele chake katika uwanja wa Maisara.

Kulia ya Balozi Seif Ali Iddi ni Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo na Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Juma Malik Akil.

Picha na – OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba ukaidi unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu Mitaani kuendelea kukiuka maagizo ya Wizara ya Afya na kufanya biashara za vyakula ovyo unaweza kuiangamiza jamii mara moja dhidi ya maradhi ya Kipindu pindu yanayoonyesha kuongezeka kwa kasi kila kukicha.


Alisema kutokana na janga hilo jamii kwa sasa inalazimika kuwa makini katika kujigomba yenyewe kuelekea kwenye utekelezaji wa maagizo na ushauri wa wataalamu wa afya bila ya kuisubiri Serikali kuu kuchukuwa hatua za kupambana na wale wanaokiuka yaliyopigwa marufuku kuyafanya kwa wakati huu.


Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani mara baada ya kuyaongoza matembezi ya maalum ya maadhimisho hayo yaliyoanzia mbele ya Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Mazizini na kuishia katika viwanja vya michezo Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.


Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina nia mbaya ya kumkomoa mtu au mfanyabiashara kutokana harakati zake za kujitafutia riziki bali lengo lake ni kunusuru maisha ya Watu kutokana na mripuko wa maradhi ya Kipindu pindu unaoendelea kuangamiza maisha ya Wananchi kila wakati.


“ Jamii bado kaidi katika kutekeleza ushauri unaotolewa na Wataalamu mbali mbali kwani wamekuwa na tabia wanapoelekezwa kwenda kulia wao hupinga na kuelekea kushoto jambo ambalo linanisikitisha sana ”. Alisema Balozi Seif.


Aliwataka wananchi wote katika maeneo yao kuchukuwa juhudi ya tahadhari dhidi ya mapambano ya maradhi hayo ya kuambukiza kwa kuondosha vyianzio vya maradhi hayo ikiwa ni pamoja na vidimbwi vya maji machafu ya kinyesi pamoja na kuchemsha maji ya kunywa.


Alisema licha ya kwamba Wananchi kipindi hichi wanaadhimisha siku ya Malaria Duniani lakini pia ni vyema wakawa na tahadhari ya kukumbuka kujilinda na matatizo ya Kipindu Pindu kinacholeta fadhaa kwa sasa kwenye mitaa tofauti hapa Nchini.


Akizungumzia siku ya Malaria Duniani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema alisimia 55% ya wagonjwa wa Malaria wanaoripotiwa katika Vituo vya Afya katika kipindi hichi ni wale wanaosafiri kutoka Zanzibar na maeneo mengine ya nje ya Visiwa hivi.


Balozi Seif alisema kwa vile maambukizo ya malaria kwa mfumo huu hayataweza kuondoka kabisa, Hivyo aliwaomba ni vyema kwa wasafiri wote kutumia vyandarua mahali popote wanapokwenda nje ya Zanzibar.
Alisema hatua hii muhimu inaweza kusaidia na kwenda sambamba na Mpango Mkakati wa Serikali kupitia kitengo chake cha mapambano dhidi ya malaria Zanzibar wa ondoa malaria kabisa ifikapo mwaka 2018.


Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema mpango wa kujikinga na homa ya Malaria unaendelea kufanikiwa kufuatia taaluma inayotolewa na wataalamu wa Afya kuwafikia Wananchi kupitia vyombo vya Habari.


Dr. Malik alisema huduma za uchunguzi wa malaria zimeimarika zaidi na kufikia asilimia 100% inayokwenda sambamba na upigaji dawa pamoja na utoaji wa vyandarua kwa Wananchi wakilengwa zaidi akina Mama Waja wazito na Watoto.


Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alisema wapo baadhi ya wananchi wanaoamua kutumia vyandarua vyao wakati wa msimu wa mvua za masika pekee jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.


“ Hadi sasa nyumba zipatazo 90,000 Unguja na Pemba tayari zimeshapigwa dawa na Watu wapatao Laki 459,000 wamepata kuchunguzwa homa ya Malaria hadi mwaka 2015 ”. Alisema Dr. Juma Malik Akil.


Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alifahamisha kwamba katika hatua nyengine ya kupambana na homa ya Malaria ndani ya kipindi cha mwaka huu wa 2016 mpango umeandaliwa kuendelea kugawa vyandarua unaotarajiwa kuanza rasmi hapo kesho Jumatatu.


Dr. Malik alisema Mpango huo unakusudiwa kutolewa vyandarua Laki 780.000 ikilinganishwa na vyandarua Laki 216,000 vilivyotolewa mwaka 2014 na kuwafaidisha wananchi wapatao Laki 434,000.


Aliwaomba Wananchi watakaohitaji kupata huduma ya vyandarua hivyo watumie utaratibu wa kujiorodhesha majina yao kupitia kwa masheha wa shehia zao ili kukimbia usumbufu unaoweza kuja kujitokeza hapo baadae.


Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ya siku ya Malaria Duniani Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo alisema maradhi ya malaria licha ya juhudi zilizochukuliwa katika kupambana nayo lakini bado yanaendelea kuathiri wananchi na hata Taifa kwa kutumia rasilmali kubwa katika kupambana nayo.


Waziri Mahmoud alisema juhudi za mapambano dhidi ya maradhi ya Malaria ni vizuri zikaendelea kushirikisha wadau wa sekta zote lengo likiwa kufikia kuupiga vita ugonjwa huo kwa asilimia 0.05%.


Ujumbe wa Mwaka huu wa Siku ya Malaria Duniani unaoadhimishwa kila ifikapo Tarehe 25 ya mwezi Aprili kwa hapa Zanzibar unasema:- “ Ili kuondoa matatizo ya malaria kwa wanaosafiri ni vyema wakatumia vyandarua mahali popote wanapokwenda ”.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/4/2016.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link