Imeandikwa na Oscar Mbuza | Habari Leo
AKITUMIA saa 2 na dakika 45 kuzungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, Rais John Magufuli ameweza kukata kiu ya Watanzania waliotaka kujua mwenendo wa serikali yake katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ilipoingia madarakani.
Pamoja na kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa ufasaha, Rais Magufuli amedhihirisha uwezo wa kiwango cha juu wa kuhifadhi takwimu za sekta mbalimbali kichwani. Pia alidhihirisha kiwango cha juu cha sanaa ya lugha katika kuzungumzia namna masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, yalivyopatiwa ufumbuzi.
Rais alitumia nafasi hiyo kuzungumzia ahadi zake kuhusu kukuza uchumi wa taifa, kuifanya nchi kuwa ya viwanda, usimamiaji ukusanyaji wa mapato, nidhamu katika uwajibikaji, nidhamu katika matumizi na kupambana na rushwa na ufisadi.
Maeneo mengine ni ongezeko la fedha kwenye miradi ya maendeleo, uboreshaji wa miundombinu, ukuzaji wa utalii na uboreshaji wa shughuli za kilimo, uboreshaji wa vyanzo vya uhakika vya nishati, uboreshaji wa sekta ya elimu na uboreshaji wa sekta ya afya.
Akizungumzia namna serikali yake ilivyosimamia suala la ukuzaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Rais Magufuli alisema kasi ya ukuaji wa uchumi ni ya kuridhisha kutokana na mwaka uliopita kukua kwa asilimia 7.
Alisema katika mwaka huu uchumi unatazamiwa kukua kwa asilimia 7.2 huku dalili za kufikiwa kwa hilo, ikijidhihirisha katika kiashiria cha robo mbili za mwaka, ambapo umeweza kukua kwa asilimia 7.9.
“Tunaelekea kuzuri, naweza kusema bado tupo kwenye line (mstari) nzuri. Kinachotakiwa ni kuendelea kupata sapoti ya Watanzania wote. “Ukuaji wa uchumi wa Taifa letu umeifanya Tanzania kuwa nchi ya pili yenye uchumi unaokua kwa kasi baada ya Cote D’ivoire (Ivory Coast),” alisema Rais ambaye pia alisema kupungua kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 7 hadi 4.5 ni moja ya viashiria.
Hata hivyo akijibu hoja kuwa katika kipindi hicho wananchi wamekuwa na maisha magumu kutokana na fedha kutoweka mifukoni, Rais Magufuli alisisitiza; “Hela hazipo mfukoni kwa wapiga dili, na zitaendelea kutoweka, wanaofanya kazi kwa bidii ndio watakaojaa fedha mifukoni. Pamoja na kusisitiza kuwa katika uongozi wake atapigana kufa kupona katika kuhakikisha kuwa inazaliwa Tanzania mpya, Rais Magufuli pia alisisitiza; “Sijafika ninapopataka. Nataka Tanzania isiwe nchi ya kuomba misaada ila iwe nchi ya kutoa misaada.
“Mara kwa mara nimekuwa nasema, nchi hii ni tajiri, ila inategemea ni namna gani tunautumia utajiri huu tuliopewa na Mungu, kama tunataka kuipeleka nchi yetu mbele sawa, lakini kama tunataka kuirudisha nyuma sawa pia, maana kupanga ni kuchagua. “Tuna kila aina ya utajiri wa madini, yapo madini mengine ambayo hayapatikani mahala pengine popote duniani, lakini Tanzania yapo na mengine yanazidi kugundulika, ni lazima tutumie utajiri huu kwa manufaa ya Watanzania masikini.”
Kuhusu kubana matumizi serikalini, Rais Magufuli alisema serikali imeendelea kusimamia eneo hilo kwa nguvu zake zote, huku akisema yeye kama mfano ameweza kubana matumizi yake kwa safari za nje, ambapo katika safari 47 alizoalikwa amekwenda 3, ikiwa ni pamoja na kukwepa mikutano aliyowakilishwa na mabalozi.
“Mbali ya kutuma Mabalozi pia nimekuwa namtuma Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri. Nikienda mimi kama Rais, safari yangu inaweza kuwa na watu karibu 40 au 60, lakini nikituma Waziri anaweza kwenda mtu mmoja au wawili. Nafanya hivyo ili tuwe na Tanzania mpya,” alisema.
Hata hivyo, akionesha hatua hiyo kutokuwa na athari katika ukuzaji wa diplomasia ya kiuchumi na uhusiano wa kimataifa, Rais Magufuli alisema katika wakati huo ameweza kuwaalika nyumbani marais karibu saba; na kusaini nao mikataba mbalimbali ya kiushirikiano wa kiuchumi.
Akitupia jicho katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, Rais alisema eneo hilo limekuwa na mafanikio makubwa, hasa kutokana na ushahidi kuwa mara tu ilipoingia madarakani, serikali yake ilikuza makusanyo kutoka Sh bilioni 800 kwa mwezi hadi kufikia Sh trilioni 1.2, huku kiwango cha juu zaidi kikirekodiwa mwezi Septemba yalipofikia Sh trilioni 1.592.
Alisema kuimarika kwa makusanyo hayo kuliifanya serikali kuongeza fedha inayoelekeza kwenye bajeti yake hadi kufikia Sh trilioni 29.5 mwaka 2016, huku fedha zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo zikiongezwa kutoka asilimia 26 hadi kufikia asilimia 40.
Alisema fedha zilizotengwa kwenye maeneo ya kisekta, pia zimeboreka ambapo katika sekta ya miundombinu, zimetengwa Sh trilioni 5.47 na kufanya miradi inayoendelea kupewa msukumo Lakini, pia kuanza miradi mipya, ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kati ya kisasa (standard gauge), uliotengewa Sh trilioni 1 ili uanze mwaka huu katika awamu ya kwanza ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
Kwa upande wa usafiri wa anga, Rais Magufuli alisema serikali imeweza kununua ndege mpya mbili aina ya Bombardier Q 400 kwa fedha taslimu, lakini pia imeagiza ndege nyingine tatu mpya ambazo matengenezo yake yanaendelea, moja ikiwa ni Bombardier Q 400 na mbili Jet SC 300 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 137 na 150 huku asilimia 30 ya fedha za awali zikiwa zimeshalipwa na za kumalizia zipo.
“Ndege moja ya Bombardier itawasili nchini ifikapo Juni mwaka kesho na nyingine mbili zitawasili mwanzoni mwa mwaka 2018. Lakini pia tumetenga Dola za Marekani milioni 10 ili kuanza mazungumzo na Kampuni ya Boeing ili watutengenezee ndege moja kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 242, mazungumzo ya awali yataanza mwezi huu,” alisema.
Rais alisema lengo la serikali ni kuwa na ndege 7 ifikapo katikati ya mwaka 2018, zitakazowezesha kutimia kwa ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii, na hasa pale safari za ndege za moja kwa moja zitakapoanza kutoka Marekani na Beijing nchini China.
Alisema kuhusu ujenzi wa barabara na madaraja miradi inaendelea. Akizungumzia Sekta ya Kilimo, Rais Magufuli alisema Sh trilioni 1.56 zimeelekezwa katika eneo hilo huku akitoa baadhi ya mifano kama ule wa upatikanaji wa soko la uhakika la korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara, lililowezesha kupanda kwa bei ya kilo moja kutoka Sh 1,000 hadi kufikia Sh 4,000.
Alisema bei ya pamba pia imepanda hadi kufikia Sh 1,300 kwa kilo. Kuhusu Sekta ya Nishati alisema imetengewa Sh trilioni 1.3 na alitumia hadhira ya jana kuelezea baadhi ya utekelezaji wa miradi kama ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Kinyerezi 1, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 333 ambapo Dola za Marekani milioni 20 zimetolewa.
Lakini, pia ujenzi wa Mradi wa Kinyerezi II utakaozalisha megawati 240, Kinyerezi III megawati 600 na Kinyerezi IV megawati 300, na kuwezesha kuzalishwa kwa megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 kutoka megawati 1,400 za sasa.
Katika kudhihirisha kauli yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Rais Magufuli alisema hatua zimechukuliwa kwa serikali yake kuhamasisha, kukaribisha, na kutenga maeneo ya uwekezaji.
Alisema hilo linafanyika chini ya Mpango wa Ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) na si vinginevyo. Alizungumzia pia kutengwa kwa Sh trilioni 4.47 katika Sekta ya Elimu, hatua iliyowezesha kutekeleza kwa mpango wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la saba hadi kidato cha nne kwa kutoa Sh bilioni 18.77 kila mwezi.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa fedha za mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 340 katika bajeti iliyopita hadi Sh bilioni 473, hatua iliyowezesha wanafunzi wanaonufaika kuongezeka kutoka 98,000 hadi 124,00, huku pia serikali ikiongeza Sh bilioni 10 zingine na kufikia Sh bilioni 483.
Picha ⏩⏩
kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayoub Rioba wakati wa kupokea maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza mwanahabari Sammy Awami wa BBC wakati akiuliza maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi w3a mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali (TSN) Dkt. Jim Yonazi wakati akiuliza maswali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Mtangazaji Tido Mhando wakati akiuliza maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Msanii Mrisho Mpoto akiimbwa wimbo wa "SIJONZE" wakati alipokutana na wahariri kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi w3a mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.PICHA NA IKULU.
Video 1 ⏩⏩
Video 2 ⏩⏩