Home » » DKT KIJAJI AWATAKA WAFANYABIASHARA KUSHUSHA BEI ZA BIDHAA ZILIZOPANDISHWA KIHOLELA

DKT KIJAJI AWATAKA WAFANYABIASHARA KUSHUSHA BEI ZA BIDHAA ZILIZOPANDISHWA KIHOLELA

Written By CCMdijitali on Tuesday, February 8, 2022 | February 08, 2022

 

Waziri wa Uwekezaji,  Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

Waziri wa Uwekezaji,  Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

 

Waziri wa Uwekezaji,  Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewataka wazalishaji wa vifaa vya ujenzi, wasambazaji na wafanyabiashara kushusha mara moja Bei ya bidhaa hizo walizopandisha kiholela bila sababu za msingi ambayo imepelekea kumuumiza mlaji wa chini.

Agizo hilo ni matokeo ya tathimini iliyofanyika ambayo ilibaini kuwa ongezeko holela la bei ya vifaa vya ujenzi  hususani saruji na nondo ambalo linasabishwa na wazalishaji wa bidhaa husika kutokuwa na mfumo wa wazi.

Waziri Kijaji ameyasema hayo tarehe 7 Februari, 2022 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akiongea na vyombo vya Habari ambapo pia alisema agizo hilo pia  linawahusu wazalishaji na wasambazaji wa vinywaji baridi.

Alisema kuwa tathimini iliyofanyika imeonesha kuwa gharama halisi za uzalishaji wa saruji haiakisiwi katika bei ya saruji iliyopo sokoni ikilinganisha na uwiano huo Katika Nchi jirani, na kwamba ongezeko la Bei ya saruji na nondo halina uwiano halisi na gharama za usafirishaji na usambazaji.

"Utafiti wetu umegundua kuwa Kuna ucheleweshaji wa makusudi wa utoaji saruji kutoka viwandani kwenda kwa wasambazaji na wanunuzi wa ndani hususani wale wasambazaji na wanunuzi wadogo ambao tayari wanakuwa wamekwisha lipia saruji husika na kuweza kusababisha wao kupandisha bei " Alisema Dkt. Kijaji.

Aidha kupitia utafiti huo ametoa maagizo kwa mamlaka zote za udhibiti kuchukua hatua kali dhidi ya walimbikizaji na wauzaji kupitia mlango wa nyuma (black market) wanaosababisha bei za bidhaa sokoni kupanda  ili kuhakikisha bidhaa zinafika sokoni Kwa wakati na kwa bei shindani ambayo haina maumivu kwa wananchi.

"Kwa kuwa kitendo cha kupanga bei kati ya washindani ni uhujumu uchumi nawaagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kukaa na kupanga bei kwa bidhaa kwa mujibu wa sheria za Nchi yetu"


"Ninawaelekeza wazalishaji kuzalisha bidhaa hizo kulingana na uwezo uliosimikwa kwenye viwanda vyenu ili kukidhi mahitaji ya soko ndani ya Taifa letu na kuwa na uwezo wa kuuza nje ya mipaka yetu ." Alisema Dkt. Kijaji.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link