Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman
Abdulla amewataka Wakuu wa Mikoa wote kuzisimamia fedha zilizotengwa kwa zoezi la utambuzi wa
Anwani za Makazi ili zitumike kama zilivyokusudiwa.
Mhe. Hemed ameeleza hayo katika Kikao Kazi
kilichowakutanisha Wakuu wa Taasisi za Serikali kuhusu utekelezaji wa Mfumo wa
Anwani za Makazi na Postikodi Zanzibar kilichoketi Ukumbi wa Sheikh Idriss
Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua
kutenga Fedha isiyopungua Billioni 28 kwa zoezi la utambuzi wa Anwani za
Maakazi ambapo zitaelekezwa kwa Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote nchini na kueleza
kuwa Mgao wa fedha hizo unazingatia na Ukubwa wa mkoa na wakaazi wake.
‘’Mgao wa fedha hizi umezingatia ukubwa wa Mikoa na uhalisia wa Idadi ya wananchi waliopo katika kila Mkoa’’Mhe. Hemed
Amesema Serikali haitamvumilia mtu yoyote atakaejaribu
kutumia fedha hizo kwa matumizi mengine sheria itachukua mkondo wake
Makamu wa pili wa rais ametaka wakuu wa taasisi husika
kuheshimu fedha hizo ili zoezi lililopangwa liweze kufikiwa na kukamilika kwa
wakati uliopangwa na liweze kuleta tija kwa nchi yetu.
‘’Fedha hizi ziende zikatumike zilivyokusudiwa na tutazifatilia kwa karibu kuona zinatumika zilivyokusudiwa’’ alisema
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka watendaji wanaosimamia
Mfumo huo kutumia Taaluma zao pamoja na Busara ili kuwafikia wananchi wote ili
waweze kutoa mashirikiano na kuweza
kukamilika kwa zoezi hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi hao
kuwajibika katika maeneo yao kulingana na
nafasi zao katika taasisi na kuwataka kuendelea kuwaelimisha wananchi
umuhimu wa zoezi hilo ili waweze kushiriki kikamilifu.
Mhe. Hemed amesisitizi kushirikishwa kwa wananchi katika
maeneo yao wakati wa utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi ili waweze
kuwajibika kikamilifu katika utambuzi wa maeneo yao na kurahisisha kukamilika
kwa mfumo huo.
Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa mfumo
huo kutoa taarifa kwa Mamlaka husika kwa changamoto zozote zile watakazokutana
nazo katika maeneo yao ya kufanyia kazi ili kuweza kutatuliwa changamoto zao
kukamilisha zoezi hilo na likamilike kama lilivyopangwa.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote kuzisimamia Kamati walizoziunda juu ya usimamaizi wa Sensa Ya watu na makazi ili kufanikisha zoezi hilo kwa urahisi zaidi.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera,
Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Dkt Khalid Salum Muhamed ameeleza kuwa ni
vyema kwa wananchi kujenga uelewa zaidi juu ya Programu hiyo kwa malengo
yaliyokusudiwa na kuwataka wadau husika kuendeleza kuelimisha jamii juu ya
umuhimu wa jambo hilo.
Aidha Waziri Dkt Khalid ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa
kuanzisha dhana ya kuwepo kwa Anwani za Makazi kwa maslahi ya watanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari Mhe. Nape M. Nnauye (MB) amemuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kuwa Wizara anayoisimamia ikishirikiana na Wizara yaujenzi Mawasiliano
na Uchukuzi Zanzibar inaendelea na zoezi hilo ambapo amemuahidi kuwa
litakamilika kwa wakati na kwa lengo lililokusudiwa.
Amesema wizara hizo zinasimamia vyema zoezi hilo kwa lengo
la kuifikisha Tanzania kukuwa kiuchumu kwa njia za kidigitali ili kuendana na
Dunia ya kidigitali.
‘’zoezi hili ni mwanzo wa safari ya kuelekea katika Tanzania ya kidigitali’’ amesema
……………………………..
Abdulrahim khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/02/2022.