Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla |
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano ili
kufanikisha Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi.
Mhe. Hemed
ameeleza hayo wakati akitoa Salamu katika kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa
kuhusu Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi kilichofanyika Ukumbi
wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.
Amesema
kukamilika kwa mfumo huo ni tija kwa Taifa ambapo itasaidia kuweza
kufikia dhamira ya Serikali ya kuwa na Maendeleo endelevu.
Aidha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kukamilika kwa zoezi hilo
itasaidia kurahisisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa
kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ambapo kukamilika kwa zoezi hilo
kutasaidia Makarani wa Sensa hiyo wataweza kutumia mfumo huo kwa
kuwaongoza kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.
Sambamba na
hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi ni la
kihistoria ambapo ni vyema kwa wahusika na wataalamu kwa ujumla
kuzingatia maelekezo wanayopewa ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Kikao
hicho kimeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Philip Isdor Mpango,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa, Mawaziri kutoka SMT na SMZ, Wakuu wa Mikoa na viongozi mbali
mbali wa Serikali.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
08 Februari 2022