Muonekano wa mashine ya CT SCAN iliyofungwa Hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani Pemba, ambayo iyasaidia kupunguza wagonjwa kufata huduma hiyo nje ya Kisiwa hicho. |
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa skuli ya kwale wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maedeleo inayojengwa kwa fedha za mkopo wa IMF. |
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua
kuwapa Wakandarasi wazawa kujenga
majengo ya miradi ya serikali ili kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ya Awamu ya Nane
inayoongozwa na rais Dr. Hussein Ali MWINYI.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo wakati wa muendelezo wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoa wa Kusini Pemba inayojengwa kwa fedha za mkopo wa IMF.
Amesema ni Imani ya serikali kuwa Wakandarasi hao watasimamia ujenzi wa miradi waliyopewa kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuweza kukamilisha miradi hiyo kwa kiwango na kwa wakati uliopangwa.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali imeelekeza fedha hizo katika ujenzi wa Skuli na Hospitali maeneo ambayo yanawagusa moja kwa moja wananchi wa Zanzibar ili kumaliza tatizo la huduma hizo ambalo lilikuwa likiwakabili wananchi wa Zanzibar kwa muda mrefu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefurahishwa kuona wazawa wa maeneo husika wanapewa kipaumbele katika kujenga miradi hiyo hali ambayo itasaidia kuwapatia kipato halali na kuwataka wakandarasi husika kuwapa stahiki zao zote kwa wakati ili kuondosha changamoto ya kujikumu.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewaasa viongozi mbali mbali kutoa ushirikiano wao katika kusimamia Miradi hiyo ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025 iliyoahidi kumaliza tatizo la uhaba wa madarasa ya kusomea pamoja na Hospitali kwa kujenga majengo ya kisasa na ya kutosheleza yenye huduma stahiki kwa wananchi.
Akigusia kuhusu suala la fedha za miradi hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali haitamvumilia yoyote atakaejaribu kufanya ubadhirifu wa fedha hizo na kuzitaka Wizara husika kuzisimamia ili zitumike kwa mujibu wa maelekezo waliyokuwemo katika mkataba.
Kwa upande wao wananchi wa maeneo yalionufaika na Miradi hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dr Hussein Ali Mwinyi kwa kuwasogezea huduma hizo muhimu karibu na maeneo yao ya makaazi ambapo ilikuwa ndio kilio chao kikubwa.
Aidha wananchi hao wameiomba Serikali kuwaandalia maeneo Mbadala kwa ajili ya shughuli ya kilimo ili kuweza kujikimu kimaisha.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea nakukagua Bohari Kuu ya Dawa Pemba ambapo hakuridhishwa na mwenendo wa Bohari hiyo na kumuagiza Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha Dawa zinakuwepo za kutosha kisiwani Pemba ili kuondosha changamoto ya Dawa kisiwani humo na kuongeza kuwa Serikali itasimamia upatikanaji wa kutosha wa huduma hizo kwa wananchi wake.
Mapema asubuhi Mhe. Hemed ametembelea Hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani Pemba kujionea huduma ya CT Scan iliyofungwa Hospitali hapo wiki mbili zilizopita iliyogharimu Zaidi ya Dolalaki saba za Kimarekani.
Katika ziara hiyo Mhe. Hemed amemuagiza Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya kuhakikisha wanamuhamisha Mtaalamu Mmoja wa Mionzi kutoka Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja na kupangiwa kazi katika Hospitali ya Abdallah Mzee Pemba ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao.
……………………….
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/02/2022