Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi. |
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika kwa Zanzibar kuanzisha Kituo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara (arbitration center), ili kwenda sambamba na hatua ya serikali ya kuvutia Wawekezaji katika miradi mikubwa.
Dk. Mwinyi amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria Zanzibar, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Amesema wakati Zanzibar ikivutia Wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha miradi mikubwa, haitokuwa busara kwa migogoro inayojitokeza kusikilizwa katika mahakama za kawaida au kwenye vituo vilioko nje ya nchi, hivyo akashauri kuanza kutungwa sheria juu ya jambo hilo.
Alisema ni vyema kuwepo sheria na mifumo ya utoaji haki itakayoweza kuvutia wawekezaji na kuweka vitega uchumi vyao hapa nchini na kutoa ajira kwa wananchi.