Katibu
Mkuu Prof. Godius Kahyarara ameitembelea kamati maalumu iliyoundwa
ikishirikisha taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kutengeneza
mfumo wa kielektroniki wa huduma za pamoja kwa wawekezaji unaojulikana
kama Tanzania Electronic Investment Window – TeIW.
Prof.
Kahyarara amesema kuwa utengenezwaji wa mfumo huu ni utekelezaji wa
agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan alilolitoa akihitaji Wizara kuanzisha mfumo wa utoaji huduma kwa
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwa na dirisha moja la huduma.
Prof.
Kahyarara ameeleza kuwa timu hii imeanza kazi hii tangu tarehe 7
Desemba, 2021 ambapo walianza kutengeneza mfumo huu katika awamu ya
kwanza na upo katika hatua ya mwisho kukamilika na kuanza majaribio na
kwa awamu ya kwanza mfumo umeziweka pamoja taasisi saba ikiwemo NIDA,
TRA, BRELA, ARDHI, KAZI, UHAMIAJI na TIC.
Amesema kuwa awamu ya
pili ya utengenezwaji wa mfumo huu utahusisha taasisi tano zilizosalia
ambazo ni TMDA, OSHA, TANESCO, TBS na NEMC
“Faida za mfumo huu ni kuwa utasaidia upatikanaji wa vibali vyote vinavyotolewa nchini kupatikana kwa urais na kwa haraka kwani huduma zote zitapatikana kupitia dirisha moja na mwekezaji ataweza kuomba vibali husika mahali popote alipo, pia utasaidia kufuatilia hatua za maombi ya uwekezaji”. Amesema Prof. Kahyarara.
Ameongeza kwa kusema kuwa kuanza kutumika kwa mfumo huu utasaidia kupunguza urasimu, gharama na muda kwani mwekezaji atapata huduma zote kupitia mfumo huu na sio kukutana na watoa huduma.
Prof. Kahyarara ametumia fursa hii kuwashukuru wabia wa maendeleo Trade Mark East Afrika (TMEA) ambao wamefadhili kuwaweka pamoja wataalamu wa kuandaa mfumo huu.
Naye mratibu wa mradi wa uaandaaji wa mfumo wa dirisha moja kwa wawekezaji (One Stop Centre) Bw. Robert John Mtendamema amesema kuwa kituo cha uwekezaji nchini kilianzishwa mwaka 1997 kikiwa na lengo la kuwahudumia wawekezaji kwa haraka chini ya mwamvuli wa dirisha moja (One stop shop) ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zinahudumia wawekezaji zimeweka maafisa ambao wana uwezo wa kutoa maamuzi ya kutoa vibali hivyo.