Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba ili kuweza kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi katika sekta za viwanda, utalii, ujenzi wa miundombinu na kutoa huduma bora za afya na elimu ni lazima kuwepo na huduma ya maji safi na salama ya uhakika.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Ngazi ya Juu wa Mashirikiano katika Uwekezaji wa Sekta ya Maji Kusini mwa Afrika (GWPSA), uliofanyika katika Hoteli ya Melia, Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja ukiongozwa na Mwenyekiti wake Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa anaamini kwamba mkutano huo utatoa elimu na uzoefu kutoka kwa wataalamu mbali mbali waliojumuika pamoja ili Zanzibar nayo iweze kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.