Home » » TANZANIA YAMALIZA MUDA WAKE WA KUONGOZA VIKAO VYA IMF KWA MAFANIKIO MAKUBWA

TANZANIA YAMALIZA MUDA WAKE WA KUONGOZA VIKAO VYA IMF KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Written By CCMdijitali on Thursday, October 13, 2022 | October 13, 2022

📍Washington DC

TANZANIA imemaliza muda wake wa miaka miwili wa kuwa Mwenyekiti wa Kundi la Kwanza la Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency) katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), linalojumuisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 23 za Afrika, ambapo katika muhula wake, mafanikio makubwa yamepatikana, licha ya kukabiliwa na changamoto za UVIKO-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. @mwigulunchemba , amesema hayo Jijini Washington D.C, nchini Marekani, baada ya kuongoza mkutano wake wa mwisho Mawaziri na Mgavana wa Kundi hilo na kukabidhi rasmi uongozi wa miaka mingine miwili kwa Namibia kama Mwenyekiti na nchi ya Botswana kama Makamu Mwenyekiti.

Katika kipindi cha uongozi wa Tanzania, Kundi hilo limenufaika kwa ongezeko la upatikanaji wa rasilimali fedha kwa nchi wanachama wake na kuwa na sauti zaidi katika shughuli za uendeshaji za Shirika la Fedha la Kimataifa (@the_imf ). 

Nafasi ya Tanzania katika kundi hilo iliwezesha kuimarisha mashirikiano kati yake na IMF ambapo imeshudiwa Shirika hilo likiongeza uwekezaji wake nchini kwa takriban shilingi trilioni 1.3. zilizotolewa kama mkopo usio na riba kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika sekta za elimu, afya, maji na utalii hivi karibuni.

Aidha, katika kipindi hicho, IMF iliidhinishia Tanzania mkopo nafuu wenye thamani ya jumla ya shilingi trilioni 2.7 za kukabiliana na athari za UVIKO-19 na vita ya Ukraine ambapo tayari kiasi cha shilingi bilioni 347 zimeshatolewa ili kuleta ahueni kwa wanachi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. 

Alisema kuwa ajenda kubwa ya mkutano huo ambao aliuongoza kwa mara ya mwisho, ilijikita katika kutafuta namna IMF inavyoweza kuzisaidia nchi wanachama kukabiliana na uhaba wa chakula na mfumuko wa bei uliosababishwa na athari za UVIKO-19, vita vya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabia nchi.






Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link