- Atoa maagizo kwa Wizara ya Madini
- Asema Mkoa wa Geita ni kinara wa dhahabu
- Asisitiza viwanda vya kusafisha dhahabu kisasa vipo hapa Tanzania
- Serikali kuangalia upya tozo zinazotozwa katika viwanda vya kusafisha madini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuendelea kufanya vizuri katika kuisimamia Sekta hiyo hapa nchini ili iwe chachu ya kitovu cha uchumi.
Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Geita katika uwanja wa shule ya msingi Kalangalala Rais Samia amesema Wizara ya Madini inafanya vizuri katika usimamizi wa Sekta hiyo lakini inapaswa kuongeza bidii hususan katika kutoa elimu ya Sheria na Kanuni za madini kwa wachimbaji.
Aidha, amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa wananchi wa mkoa wa Geita katika ujenzi wa uchumi hususan kwa kupitia shughuli za uchimbaji wa madini.
"Ni kweli kabisa kiwango kikubwa cha madini ya dhahabu kinapatikana hapa Geita na inachimbwa ndani ya mkoa wa Geita, mchango wa mkoa wa Geita ni zaidi ya asilimia 50 ya dhahabu yote inayochimbwa Tanzania," amesema Rais Samia.
Mara baada ya kuzindua kiwanda cha kusafisha dhahabu, Rais Samia amewataka wanachi wa Geita na mikoa yote inayochimba madini ya dhahabu kuvitumia viwanda vya kisasa vya kusafisha na kuchenjua dhahabu vilivyopo nchini mara baada ya kuzindua kiwanda cha Mama Masasi cha Geita.
"Niombe sana tupeleke dhahabu zetu huko zikachenjuliwe ili Tanzania iongeze thamani ya madini ya dhahabu yenye thamani kubwa," amesisitiza.
Vile vile, ameiagiza Wizara ya Madini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara za madini zinafanywa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia Sekta ya Madini.
Vile vile, Rais ameitaka wizara kuendelea kutoa elimu juu ya Sheria ya Madini na Kanuni zake kwa wadau mbalimbali kupitia mafunzo maalum.