Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa kwa maandalizi mazuri ya Kongamano la Uwekezaji mkoani humo litakaloibua fursa za uwekezaji na kukuza uchumi wa mkoa.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Desemba 19, 2024 mkoani Kagera wakati akizungumza katika Tamasha la Pili la Uwekezaji la mkoa huo ikiwa sehemu ya Wiki ya Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani).
“ Nawapongeza waandaaji wa Kongamano hili na kama kuna watu wamekuja kuwekeza hapa napenda kuwapongeza wale mlioitikia wito tangu kwenye kongamano la kwanza na kuja kuwekeza hapa,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Maombi yangu baada ya mkutano huu waje wengine kuwekeza na tutumie fursa hii ya uwepo wa mkoa huu kijiografia na kutumia fursa zilizopo,”
Aidha, amewaasa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa na kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.