Na. Hellen M. Minja, Habari – DODOMARS
Kufuatia wimbi la wizi wa vifaa vya miundombinu ya Taasisi za Serikali, agizo limetolewa kwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma kukaa na kupanga mkakati wa namna ya kukabiliana na changamoto hiyo inayowagharimu wananchi kwa kukosa huduma za msingi, lakini pia kuitia Serikali hasara kubwa.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa kikao cha kwanza kwa mwaka 2024/2025 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dodoma kilichofanyika Disemba 18, 2024 katika ukumbi wa ofisi yake Jijini Dodoma.
“Suala la wizi wa miundombinu linasikitisha sana, si kiashiria kizuri kuendelea kukifumbia macho na tupeane majukumu, wakuu wa Wilaya nendeni katika Wilaya zenu mkakae, mje na mikakati ya namna gani mnakwenda kukabiliana na wizi wa miundombinu ya Serikali na ninawapa muda, mpaka mwishoni mwa mwezi Desemba ” Mhe. Senyamule.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kushirikisha Wananchi kwenye miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kila mmoja awe sehemu ya miradi hiyo kwani wao ndio wanufaika na walinzi pia.
“Kuna utaratibu ambao upo kwenye miradi ya Serikali unaosema, kila mradi unapokwenda kwenye Kijiji, Kata, ni lazima wananchi washirikishwe kwenye mradi husika, lazima taarifa ibandikwe kwenye Serikali ya kijiji, ofisi au Kata ili kila mwanakijiji ajue na awe sehemu ya mradi” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Akizungumzia hali ya Barabara za Mkoa hasa kipindi hiki cha mvua, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS, Mhandisi Zuhura H. Amani amesema;
“Sehemu kubwa ya mtandao wa barabara za Mkoa ziko katika hali nzuri,isipokua baadhi ya barabara ambazo ziliharibiwa na mvua hali iliyosababisha baadhi ya maeneo kutopitika ,na mengine kupitika kwa shida. Hadi kufikia mwishoni mwa Novemba, 2024, matengenezo ya kuimarisha au kurudisha mawasiliano yamefanyika na mengine yanaendelea” Mhandisi Zuhura.
Katika wasilisho la Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA),pamoja na mambo mengine, lilizungumzia mapitio ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.