Home » » Mkutano wa 14 wa Mapitio na Mpango wa pamoja wa Utekelezaji katika Sekta ya Afya - ZANZIBAR

Mkutano wa 14 wa Mapitio na Mpango wa pamoja wa Utekelezaji katika Sekta ya Afya - ZANZIBAR

Written By CCMdijitali on Thursday, February 20, 2025 | February 20, 2025

 Na   Rahma Khamis Maelezo  20/2/2025

 

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed Suleiman Abduulla amewataka watoa huduma za afya kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ili kupunguza malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi yao.

 

Wito huo ameutoa  katika Ukumbi wa Madinat - Albahr Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akifungua  mkutano wa 14 wa Mapitio na Mpango wa pamoja wa Utekelezaji katika Sekta ya Afya.

 

Amesema kufanya kazi  kwa  bidii na nidhamu ni kufuata msingi wa maadili ya kazi ya utoaji wa huduma za afya kutasaidia kupunguza malalamiko  yanayotolewa na baadhi ya hudumu  wakati wa kuwahudumia wagonjwa.

 

Mhe. Hemed amewaomba Washirika wa Maendeleo kuelekeza nguvu zao katika kuisaidia Wizara ya Afya kwa kuweka miundombinu ya kidijitali ya ukusanyaji wa taarifa za afya ili juhudi zinazochukuliwa na Serikali na Wadau ziweze kutatua changammoto ikiwemo ya upatikanaji wa taarifa sahihi za takwimu za afya.

 

Naye Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwa bila ya kuimarisha afya ya msingi hawatafikia malengo hivyo wataendelea kuimarisha miundombinu na vifaa tiba vya kisasa ili kutoa huduma bora kwa jamii.

 

Waziri Mazrui ameeleza kuwa vifo vya watoto vimepungua kutoka 1940 kwa  mwaka 2023 hadi kufikia  1847 kwani lengo la Serikali ni kupunguza vifo vya mama na mtoto

 

Aidha amewasisitiza madaktari na  wataalamu wa Afya kubuni miundombinu bora itakayoweza kuwasaidia mama wajawazito ili kupunguza kifafa cha mimba sambamba na kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dkt Amuor Suleiman amesema kuwa kwa mwaka 2022 hadi 2024 Wizara imefanikiwa kutoa huduma za afya katika vituo vya ngazi ya chini (vituo vidogo) pamoja na kuanzisha mfuko wa huduma za afya kwa ajili ya kutoa huduma bora nchini ambapo Serikali imetenga   bilioni 344 kwa Sekta ya Afya ili kuimarisha afya za wananchi.

 

Aidha amefahamisha kuwa Wizara  imefanikiwa  kuzalisha hewa tiba pamoja na kununua Magari makubwa ambayo yanatoa huduma za afya, ambulance  kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii, kununua vifaa vya kugundukia maradhi yanayowakabili wananchi ikiwemo kansa Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarika.  

 

Akizungumzia maradhi yanayoongoza hadi kufikia sasa ni pamoja na maradhi ya mfumo wa hewa, maradhi ya kuharisha pamoja maradhi ya UTI, ipo haja ya kutilia mkazo kwa mwaka ujao ili kupunguza matatizo hayo.

 

Dk Amour ameeleza kuwa kwa upande wa watoto chini ya miaka mitano matatizo ya mfumo wa kupumua  pamoja na maradhi ya ngozi ambapo  maradhi yanayoongoza kusababisha vifo ni maradhi yasiyoambukiza hivyo mikakati madhubuti inahitajika ili kupunguza idadi ya vifo hivyo ikifuatiwa na  vifo vya watoto wachhanga.

 

Mkutano huo umewashirikisha wadau mbalimbali wa Afya wakiwemo washirika wa kimataifa ambapo Kaulimbiu ya mkutano huo ni "Uwepo wa Mfumo Bora wa Huduma za Afya ya msingi uliyoungwanishwa,ubunifu unaojengwa kwa ushahidi ili kufikia Upatikanaji wa Afya Jumuishi kwa wote”.



















Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link