THBUB YATEMBELEA VYUO VYA MAFUNZO YA AMALI, PEMBA
TUME ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) imefanya ziara ya kuvitembelea vyuo
viwili vya Mafunzo ya Amali vya Vitongoji, Wilaya ya Chake Mkoa wa Kusini Pemba na cha
Daya Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa lengo la kutoa elimu na
kujenga uelewa mpana kwa jamii juu ya dhana nzima ya Haki za Binadamu na Misingi ya
Utawala Bora.
Maafisa wa Tume hiyo, Ofisi ya Pemba wakiongozwa na Afisa Uchunguzi Ndg. Ramadhani Slaa
wameifunza jamii juu ya umuhimu wa kutambua Haki za Binaadamu na Utawala Bora pamoja
ushiriki na kuanzisha klabu za Haki za Binaadamu katika vyuo na kuwashauri wanafunzi wa vyuo
hivyo kujiunga na klabu hizo.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, ofisi za chuo cha Vitongoji, Bw. Slaa alieleza nia ya ziara yao
chuoni hapo mbali na kutoa elimu ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora lakini kushirikiana na
vyuo hivyo kuanzisha Klabu za Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kukuza ushirikiano na nguvu
ya pamoja kwa kuongeza uelewa kwa jamii juu dhana ya Haki za Binaadamu na misingi ya Utawala
Bora.
Aidha, Bw. Ramadhan Slaa awasihi wanafunzi vyuoni humo kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa
jamii zao katika kueneza dhana halisi ya Haki za Binaadamu na misingi ya Utawala Bora ili kukuza
jamii yenye uelewa mpana kwa maeneo hayo.
Katika hatua nyengine, THBUB ilimshauri, Mkuu wa chuo cha Daya cha Mtambwe, Mwl. Saada Ali
Hamad, kuanzisha Klabu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora chuoni hapo ili kuongeza hamasa
na uelewa zaidi kwa jamii.
Naye, Mwalimu dhamana wa Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Vitongoji na Mkuu wa Idara ya
Masomo Mtambukwa chuoni hapo, Mwl. Khamis Abdalla Khamis alitoa shukrani kwa THBUB kwa
kuwatembelea chuoni hapo sambamba na kuishauri Tume kuwa karibu na Klabu hizo ili kuzijengea
uimara na ziwe endelevu pamoja na kuahidi kuzisimamia vyema katika kuendeleza shughuli za
kutoa elimu kupitia klabu hizo.
Halikadhalika,kwa nyakati tofauti wanafunzi wa vyuo viwili hivyo, walipata nafasi ya kuuliza maswali
kuhusu dhana na uelewa wa Haki za Binaadamu na Utawala Bora pia kutaka kujua umuhimu na
faida za kujiunga na Klabu za Haki za Binadamu na Utawala Bora vyuoni humo.
Kwaupande mwengine, wanafunzi hao wameiomba THBUB kurudi tena kwenye vyuo vyao na
kujenga utamaduni wa kuwatembelea mara kwa mara ili wajifunze zaidi. Hata hivyo, waliiahidi Tume
kuongeza ushiriki wao mpana katika kusimamia na kuendeleza klabu hizo ndani ya vyuo vyao.
Kiasi cha wanafunzi wasiopungua 600 wakiwemo 400 kutoka Chuo Cha mafunzo ya Amali cha
Vitongoji na 200 kutoka chuo cha Daya, Mtambile kwa nyakati tofauti walihudhuria hafla hiyo
iliyowajenga kitaaluma na kuelezwa juu ya umuhimu wa kushiriki klabu kama hizo na umuhimu wake
wa kuanzishwa kwenye vyuo vyao.
MWISHO.