Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amewasili jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika (AU) kinachofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025.
Kikao cha Baraza la Mawaziri kilitanguliwa na Kikao cha 49 cha Kamati ya Mabalozi/Wawakilishi wa Kudumu kwenye Umoja wa Afrika kilichofanyika kuanzia tarehe 14 Januari hadi 10 Februari, 2025 ambapo vikao hivyo ni maandalizi ya awali ya Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 15 na 16 Februari, 2025.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na ataambatana na Mawaziri na Viongozi wengine Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na masuala mengine Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utachagua na kuidhinisha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika pamoja na Makamishna sita (6) wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika baada ya viongozi waliopo sasa kumaliza muda wao wa miaka 4 (2021-2025) wa kuhudumu katika Kamisheni hiyo; kuchagua na kuidhinisha wajumbe watano (5) wa Baraza la Amani na usalama la Umoja wa Afrika; Kuchagua mjumbe mmoja (1) wa Taasisi ya Anga ya Afrika; na kuchagua na kuidhinisha nafasi ya Makamu wa Rais wa Baraza la Chuo Kikuu cha Pan-African.
Uchaguzi mwingine ni wa wajumbe watano (5) wa Bodi ya Ushauri Dhidi ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika, Uchaguzi wa mjumbe mmoja (1) wa Kamati ya Wataalamu Afrika inayoshughulikia Haki na Ustawi wa Mtoto na uchaguzi na uteuzi wa wajumbe sita (6) wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika Sheria ya Kimataifa.
Vilevile, Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali utapitia na kujadili ripoti za masuala ya kimkakati ikiwemo: Ripoti ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika; Ripoti kuhusu ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa Nchi Tajiri Duniani (G20), Ripoti kuhusu Mchakato wa Mageuzi ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika na Ripoti kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Kuanzisha Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Pia utapitisha Maazimio ya Mkutano wa Sita wa Katikati ya mwaka wa Kamati ya Uratibu uliofanyika Accra Ghana, mwezi Julai 2024; na Maamuzi mbalimbali ya Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.