Home » » MAKAMU WA PILI AKIGAWA IFTAR SKULI ZA KUSINI PEMBA

MAKAMU WA PILI AKIGAWA IFTAR SKULI ZA KUSINI PEMBA

Written By CCMdijitali on Wednesday, March 12, 2025 | March 12, 2025

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka Mazingira wezeshi kwa Wanafunzi kiweza kujisomea bila ya changamoto yoyote.

 

Mhe. Hemed ameyasema hayo katika ziara ya kuwatembelea na kuwapatia Iftari Wanafunzi wanaokaa Dakhalia katika Skuli za Mkoa wa Kusini Pemba.

 

Alhajj Hemed amesema Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu na kufikia Bilioni 33 kwa mwaka wa fedha 2024/ 2025 kwa lengo la kuhakikisha kila mwanafunzi anaestahiki kupatiwa mkopo kuanzia ngazi ya Diploma hadi shahada ya uzamivu anapatiwa fursa hio.

 

Amesema kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Elimu Serikali imejenga Vyuo vya Amali katika maeneo tofauti ili kuwajengea uwezo wale ambao hawakubahatika kuendelea na Elimu ya juu ili waweze kujendelea kiuchumi

 

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Walimu kwa kuendelea kujitolea kuwasomesha Wanafunzi na kuwahakikishia kuwa Serikali imejipanga kuwaongezea maslahi zaidi pamoja na kuwaongezea ujuzi ili kuzidi kuzalisha wasomi katika Taifa la Tanzania.

 

Akitoa shukurani kwa niaba ya Wanafunzi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Fidel Castro Mwalimu Seif Hamad Khalfan amesema wameipokea sadaka hio kwa moyo mkunjufu na kuahidi wataitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili Wanafunzi waweze kusoma kwa utulivu wakiwa na uhakika wa Iftar kwa kipindi chote watakachokuwa skulini hapo hasa katika mwezi wa Ramadhan.

 

Mwalimu Seif amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa wataendelea kupambana kwa juhudi zote ili waendelee kupata matokeo mazuri kwa maslahi mapana ya wanafunzi na Taifa kwa ujumla.

 

Akitoa shukran kwa niaba ya wanafunzi wenzake Ndg. Salim Ramadhan Pandu ambae ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi kutoka skuli ya Sekondari ya Dkt. Salim Ahmed salim amemshukuru Mhe. Hemed kwa kuona umuhimu wa kuwafutarisha Wanafunzi wanaoishi katika Dakhalia ili kuondokana na changamoto ya Iftari.

 

Wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi anazozichukua katika kukuza Sekta ya Elimu nchini na kuahidi kufanya vizuri katika Mitihani yao.

 

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Mhe Hamad Omar Bakari amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuendelea kugawa Iftari kwa Wanafunzi wanaokaa Dakhalia hatua ambayo inaamsha Hamasa kwa Wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa na uhakika wa Iftari Katja mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

 

Amesema Serikali za Wilaya na Mkoa zinajitahidi kutoa mashirikiano kwa Skuli zote ili kufikia lengo la kuanzishwa kwa Dakhalia Nchini na kuwaomba wazazi na walezi kuendeleza mashirikiano ili kuzalisha Taifa lenye Elimu na maadili mema.

 

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea na kuwapatia Iftari Wanafunzi wanaokaa Dakhalia katika Skuli ya Sekondari Fidel Castro, Skuli ya Sekondari Dkt. Salim Ahmed Salim, Skuli ya Sekondari Madungu, Skuli ya Sekondari Mohamed J. Pindua na Skuli ya Sekondari kiwani.

 

…………………..

Imetolewa na Kitengo cha habari (OMPR)

12.03.2025

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi Iftari kwa Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Fidel Casro wanaojiandaa na Mitihani yao ya Kidato cha sita mwaka huu

Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Fidel Casro wanaojiandaa na Mitihani yao ya Kidato cha sita mwaka huu

Rais wa Serikali ya Wanafunzi Skuli ya Sekondari Fidel Casro Dhulkifli Ali Khatib akitoa shukurani kwa niaba ya wananfunzi wenzake katika ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kukabidhi Iftari Mkuu wa Skuli ya Sekondari Fidel Casro

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi Iftari kwa Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Dkt. Salim Ahmed Salim wanaojiandaa na Mitihani yao ya Kidato cha sita mwaka huu


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link