Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka wazazi na walezi kutoa mashirikiano kwa walimu wa Madrasa ili kusaidia upatikanaji wa Elimu bora kwa watoto.
Alhajj Hemed ameyasema hayo alipokuwa akiwasalimia Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Masjid Al Amin Kibweni alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema jamii ina uhitaji Mkubwa wa wasomi wa Masomo ya kidini na ya kidunia hivyo, ni vyema kwa wazazi kutoa mashirikiano kwa walimu wa Madrasa ili kupata kizazi chenye hofu ya Mungu hatua ambayo itapelekea kumaliza vitendo viovu katika Jamii.
Aidha Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Mskiti huo kwa kuwa na kawaida ya kuwasaidia Mayatima hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan jambo ambalo linasaidia kuingiza furaha kwa watoto hao ambao hujihisi wapo sawa na watoto wengine.
Amesema Uislamu umeeleza Faida nyingi anazopata anaemhurumia Yatima ikiwa ni pamoja na kuwa karibu Peponi na Mtume Muhammad (S.A.W) na kuwataka Waumini kuendeleza jambo hilo kwa Kila hali ili kufikia lengo la kuanzishwa kwake.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameendelea kuwakumbusha Waislamu na wazanzibar kwa ujumla umuhimu wa kulinda Amani na Utulivu uliopo ili kutoa fursa kwa Serikali kuendelee kuwaletea maendeleo Wananchi wake.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amepokea kilio cha Wananchi hao kuhusu barabara inayotaka KMKM Kibweni Hadi Mwanyanya na kuwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya nane inayoongozaa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imepanga kuzijenga barabara zote kwa kiwqngo cha Lami ili kuwaondolea usumbufu Wananchi.
Akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa Shekh Yussuf Muhammed Yussuf Ameeleza kuwa Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa kuzidisha Ibada na kujikurubisha na Allah na kuachana na mambo yote yenye kupunguza fadhila za mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Amesema Mwezi wa Ramadhan ni Msimu pekee ambao M/Mungu (S.A.W) huwa karibu na waja wake hivyo, ni vyema Kila mmoja kuutumia vyema Msimu huu ili kupata kheri na Fadhila zinazopatikana ndani yake.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amemtembelea na kumjuulia hali aliewahi kuwa Diwani wa Magomeni Bi Arafa Mohammed Said (G7) Nyumbani kwake Mwanyanya Wilaya ya Magharibi 'A'
…………………………...
Abdulrahim Khamis
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
07/03/2025