MIUNDOMBINU YA ELIMU ZANZIBAR SASA YALINGANA NA MAHITAJI YA KARNE YA 21

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mazin...

Latest Post

NAIBU KATIBU AFUNGA MAFUNZO YA WAONGOZAJI WATALII MARUHUBI

Written By CCMdijitali on Friday, March 7, 2025 | March 07, 2025

 Na Ali Issa Maelezo 7/3/2025

 

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar  Amina Ameir Issa amewataka wahitimu wamafunzo ya kutembeza watalii nchini (tour Guider) kufuata Sheria na taratibu zilizopo ili kulinda mila na desturi za Mzazibari.

 

Ameyasema hayo katika Chuo cha Maendeleo ya Hoteli na Utalii Maruhubi wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo waongozaji watalii kukuza utamadni na kuwa na maadili mema katika kazi zao.

 

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa mafunzo mfulululizo kwa waongozaji watalii ili kuona wafanyakazi wa sekta hiyo wanafanyakazi  kwa uweledi na ustadi kwa kufuata Sheria na taratibu kwa lengo la kuleta matumaini na maeendeleo nchini.

 

"Nimeambiwa Mafunzo haya mmefuzwa heshima,mmerekebishwa tabia, na maadili yetu hivyo na amiini mtakua vijana waledi kulinda maslahi ya Nchi na tamaduni zetu" alisema Naibu Katibu Mkuu.

 

Alifahamisha kuwa Serikali ilifanya ukaguzi katika maeneo mbali mbali ya kiutalii na kubaini kuwepo  kwa baadhi ya watembeza watalii  hawana maadili wala tabia njema katika utendaji wa kazi zao na kuamua kuwapatia elimu vijana  hao ili kuwajenga katika maadili, silka na utamaduni  za Mzazibari.

 

Aidha aliwataka kuwa mabalozi kwa wengine pamoja na kusambaza elimu hiyo ambapo matumaini yao kuona utalii unaendeshwa na watu waledi na kuipa sifa nchii na kukuza uchumi wa nchi.

 

Mapema Mkurugenzi Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Dkt. Abdalla Muhamed alisema Mafunzo kama hayo wameshawahi kutoa katika maeneo mbalimbali ya utalii nchini ikiwemo Paje, Matemwe, Jambiani na Maruhubi ambapo mafunzo  kama hayo wanatarajia kuyatoa katika Kisiwa cha Pemba wiki ijayo.

 

Nae mshiriki wa mafunzo hayo Ahlam Abdalla Ali kutoka Magogoni aliishukuru Serikali ya awamu ya nane na Benki ya NMB Foundation kwa kuwapatia Mafunzo hayo na kuahidi kuifanyia kazi elimu waliyoipata na kutokwenda kinyume na sharia na taratibu ziliwekwa        ili kuipa hadhi na heshima nchi kupitia Sekta ya utalii.

 

Mafunzo hayo ya siku tatu (3) yamewashirikisha vijana150 wakiwemo watembeza watalii  ambapo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo historia ya Zanzibar na watawala waliowahi kuingia zanzibar.

 


Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar  Amina Ameir Issa


WAZIRI MKUU AONGOZA MATEMBEZI HISANI NA UZINDUZI WA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA TET

  •  Ausisitiza uongozi kuongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu


  • Ampongeza Rais Dkt. Samia kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza matembelezi ya hisani na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TET) ambapo amesisitiza uongozi wa taasisi hiyo kuongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwenye shule zote nchini.

Waziri Mkuu amesema anafahamu kuwa TET imedhamiria kuchapa vitabu kwa wingi ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, jambo ambalo litaleta  manufaa makubwa katika elimu na Taifa kwa ujumla. “Hivyo, kwa dhamira ya dhati kabisa, sote hatuna budi kuliunga mkono jambo hili.” 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 7, 2025) alipozungumza baada ya kumalizika kwa matembezi ya hisani katika ofisi ya TET, Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu nchini. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na TET kutumia matembezi ya hisani kuchangisha fedha za kuchapisha vitabu ni vema kwa uongozi wa taasisi hiyo ukaongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwa kushirikisha kampuni za uchapishaji na wadau wa sekta binafsi ili kupunguza gharama za uchapishaji. 

Amesema ushiriki wa wadau katika uchapishaji wa vitabu utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu shuleni, na kufikia lengo la kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. “Vitabu ni chanzo cha maarifa na maendeleo, na ni muhimu katika kuhakikisha elimu bora kwa wanafunzi.” 

Akizunguzmia kuhusu kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema kitabu kimoja mwanafunzi mmoja, Waziri Mkuu amesema inawiana na malengo ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa watoto wa Tanzania wanapata elimu bora. “Kupitia elimu bora, Taifa linaweza kufikia malengo yake ya maendeleo endelevu na kuboresha ustawi wa jamii.” 

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba alisema maadhimisho ya miaka 50 TET pamoja na kampeni ya kitabu kimoja mwanafunzi mmoja yanatarajiwa kuhitimishwa Juni mwaka huu. “Maadhimisho haya yanalenga kukusanya shilingi bilioni 297 kwa ajili ya kufikia azma ya kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja na ununuzi wa kompyuta za kuhifadhi vitabu.”









TAASISI NA MASHIRIKA ZATAKIWA KUWAJIBIKA KUCHANGIA JUHUDI ZA SERIKALI KATIKA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI

Written By CCMdijitali on Thursday, March 6, 2025 | March 06, 2025

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Viongozi wa Taasisi na Mashirika wanawajibika kuchangia juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuandaa na kutekeleza mikakati itakayosaidia kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni unaofanyika katika Ukumbi wa APC – Mbweni Jijini Dar es Salaam. Amesema Mikakati itakayoandaliwa ni vema ijielekeze katika kuhimiza matumizi bora ya rasilimali, uwekezaji katika nishati mbadala na teknolojia rahisi na nafuu, na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. 

Kuhusu Biashara ya Kaboni, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuwepo kwa uratibu madhubuti katika utekelezaji wa biashara ya kaboni kwa kuwa biashara hiyo inahusisha wadau wengi. Ameongeza kwamba ni vema Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Serikali za Mikoa kukutana kwa ajili ya kujadili na kupata mwelekeo wa pamoja katika uendeshaji wa biashara hiyo. 

Pia Makamu wa Rais amesema ni muhimu kupata uzoefu kuhusu uendeshaji wa biashara ya kaboni kutoka nchi nyingine ili kuona namna zinavyokabiliana na changamoto zinazojitokeza. 

Makamu wa Rais amesema uwazi katika mikataba ya biashara ya kaboni utasaidia uendeshaji wa biashara hiyo na kuondoa hali ya kutoaminiana. Amesema kwa sehemu kubwa, uendeshaji wa biashara hiyo umetawaliwa na Madalali ambao pia utaratibu wa upatikanaji wao hauko wazi. Ameongeza kwamba kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kufahamu kilicho ndani ya mikataba kati yao na wanunuzi na kama kiasi kinacholipwa ndicho kilichotolewa na wanunuzi. 

Makamu wa Rais amesema taratibu za jinsi biashara ya kaboni inavyofanyika zinapaswa kuwekwa wazi kwa wadau wakuu, yaani Wanavijiji na Halmashauri, ambao ndiyo wamiliki wa misitu. Amesisitiza Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na TAMISEMI kuongeza kasi ya kufanya programu maalum ya kufikisha elimu katika ngazi ya wilaya na vijiji. Pia ameviagiza Vyombo vya Habari na Taasisi za Teknolojia kuongeza jitihada katika kutoa elimu ya biashara ya kaboni. 

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza taasisi na mashirika kutekeleza mipango ya kutumia vifaa vyenye matumizi kidogo ya umeme na kuhamia kwenye magari yanayotumia umeme na gesi. Amewasishi Wakuu wa Mikoa kuahamasisha vyombo vya ulinzi na usalama katika mikoa kuanza kutumia magari yanayotumia nishati ya umeme na gesi. Amesema ni muhimu taasisi na mashirika yawe na vitengo vya mazingira na kutenga bajeti za utekelezaji wa miradi na shughuli za kuhifadhi mazingira. 

Makamu wa Rais amesema Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kukuza mchango wa biashara ya kaboni katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo kiuchumi. Amesema kupitia Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (National Carbon Monitoring Centre) hadi mwishoni mwa mwezi Februari 2025, kimesajili miradi 72. Amesema pia miradi mikubwa katika sekta ya usafirishaji kama mradi wa Treni ya Mwendokasi (SGR) na Mabasi ya Mwendo kasi kwa Jiji la Dar es Salaam, miradi ya Mionzi ya Jua, nishati safi ya kupikia na hata wa bwawa la umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambayo inachangia katika utekelezaji wa michango ya taifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, inaweza kusajiliwa katika fursa ya biashara ya kaboni kwa kufuata taratibu na miongozo husika. Aidha amesema ipo fursa ya kutumia taka ngumu katika biashara ya kaboni ili kunusuru hali ya uchafuzi wa mazingira na kukuza uchumi wa Taifa. 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Masauni amesema uwepo wa Kituo cha Kusimamia na Kuratibu Kaboni kisheria (NCMC) utaleta manufaa mbalimbali ikiwemo kutoa fursa kwa nchi kushiriki katika masoko ya kaboni kimataifa na kuchochea uwekezaji katika sekta zingine. 

Amesema manufaa mengine ni kuongeza pato la Taifa, kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira pamoja na kuimarisha ushirikiano na Taasisi, Mashirika na Sekta Binafsi katika kuibua fursa za uwekezaji za biashara ya kaboni nchini. Ameongeza kwamba, kwa sasa kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuingia mikataba mbalimbali itakayoleta faida kwa Taifa bila kipingamizi cha kisheria. 

Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman amesema Mkutano huo ni muafaka katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa Zanzibar kama ilivyo kwa maeneo mengine, inaendelea kuathirika na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaikumba Dunia. Amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri mashamba ya kilimo kuingia maji ya chumvi, kuharibika kwa ubora wa maji ardhini unaotokana na visima vya maji kuingia maji ya chumvi, kupanda kwa kina cha maji ya bahari kunakopelekea kuongezeka kwa mmonyoko wa fukwe na kupotea kwa makaazi ya baionuai. 

Aidha Mhe. Harusi ameongeza kwamba Zanzibar tayari imepitisha kanuni ya biashara ya kaboni hivyo Mkutano huo unatoa fursa ya kujifunza na kupata uzoefu kuhusiana na biashara hiyo.

 







Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

06 Machi 2025

Dar es Salaam.

MAWAKALA WA VYAMA KIELELEZO CHA UWAZI UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA

 Na. Mwandishi Wetu

Uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kielelezo cha uwazi na ni muhimu kwa kuwa mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.

 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo tarehe 06 Machi, 2025 wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari wa mkoa wa Dar es Salaam.

 

Jaji Mwambegele amesema licha ya umuhimu huo mawakala hao wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

 

“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.  Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima,” amesema.

 

Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesema Tume imetoa kibali kwa asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hizo, taasisi tisa ni za kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi.

 

Amewasisitiza watendaji hao kutoa ushirikiano kwa taasisi, asasi na waangalizi waliopata vibali watakapofika kwenye maeneo yao kwa kuwa ni wadau muhimu na akaongeza kuwa Tume itawapa vitambulisho kwa urahisi wa kuwatambua.

 

Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwa kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa na vinatakiwa kutumika katika awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari.

 

“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu. Aidha, mnapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza,” amesema.

 

Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari mkoani Dar es Salaam ambao utaanza tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Mwisho

 


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akijadili jambo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani (kulia) wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari wa mkoa wa Dar es Salaam yaliyoanza leo Machi 06,2025 na yanataraji kumalizika kesho Machi 07, 2025 na kufanyika Ubungo mkoani Dar es salaam. (Picha na INEC). 


--

Mroki Mroki

Online Reporter/Blogger

Mob: +255 755 373999 

Email: mrokim@gmail.com.

Blog: https://mrokim.blogspot.com/

     DODOMA, TANZANIA

WANANCHI JITOKEZENI KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimehamasisha wanachama wake kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli ya kuboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura ili kitete nafasi ya kushika dola.

Shughuli ya uboreshaji taarifa za mpiga kura zitakazo mwenzesha kila mtanzania kupata kibali cha kutumia haki yake ya kumchagua kiongozi anayemtaka inasimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na kwa mkoa wa Dar es Salaam linatarajiwa kuanza Machi 17 hadi 23 Mwaka huu.

Akihamasisha shughuli hiyo kwenye mkutano wa ndani uliofanyika Wilaya ya Ubungo, ukiwakutanisha viongozi wa Chama hicho, Jumuiya ngazi ya Shina, tawi, mitaa, Kata na Wilaya, Katibu wa NEC, Itikadi  Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla amesema ili watete dola ni lazima wafuasi wao wajiandikishe kabla ya kuanza kuwashawishi watanzania wengine.

"CCM tunawachama 12 milioni nchi nzima lakini  Dar es Salaam tunaongoza kwa idadi ya wapiga kura wengi ikilinganishwa na mikoa mingine,  tusilale mtihani tulionao kwanza kuhakikisha idadi hiyo wanajitokeza kujiandikisha viongozi wa Wilaya, Kata, Matawi , Mitaa  hadi Shina hakikisheni watu wenu wanaenda  kujiandikisha, " amesema Makalla .

Makalla mesema licha ya  kuhitaji kutetea dola lakini uchaguzi ni namba kwani anayepata kura nyingi anatangazwa mshindi hivyo wasipuuze mchakato huo kama wanataka kuitawala nchi.

"Wapiga kura wako ngazi ya chini huku wilayani ni kuratibu tu lakini watu wako kwenye mashina, tawi na Kata kwahiyo watu wa wilayani tokeni simamieni kazi hiyo mkoani na mabalozi nayie wapeni ushirikiano tusifanye makosa," amesema 

Makalla ambaye ni mlezi wa mkoa wa Dar es Salaam kupitia chama hicho amesema hataki kuona wananchi wakimuangusha kupitia shughuli ya uboreshaji daftari la mpiga kura kwani walishafanya makubwa na hapaswi kujikwaa kwa jambo hilo.

"Mkitoka hapa wekeni kwenye ratiba zetu kuanzia Machi 17 hadi 23, 2025 na nyie kama viongozi anzeni na watu wenu wanaowazunguka na baada ya hapo anzeni kuhamasisha wengine ili tujihakikishie kura katika uchaguzi mkuu," amesema.

Amesema wakati wakiendelea na majukumu hayo, viongozi wa serikali za mitaa waliochaguliwa wanatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuhakikisha ofisi zao zinakuwa kimbilio.

"Tunahitaji kuona wananchi wanapata huduma nzuri ili wafurahie hawakufanya makosa kumchaguzi kiongozi wa Chama cha mapinduzi," amesema












#CCMImara
#VitendoVinaSauti
#KaziIendelee

Tume kuandikisha Wapiga Kura wapya zaidi ya Laki sita Dar

Written By CCMdijitali on Wednesday, March 5, 2025 | March 05, 2025

 


Na. Mwandishi Wetu  

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Dar es Salaam utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025 ambapo wapiga kura wapya 643,420 wanatarajiwa kuandikishwa.
 
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhan kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Machi, 2025.

“Leo tupo hapa Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa huu, ambapo zoezi litafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 17 Machi, 2025 na kukamilika tarehe 23 Machi, 2025 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema Jaji Mwambegele.

Amesema mkoa wa Dar es Salaam ndio wa mwisho kwenye awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Dafatri ambayo ilizinduliwa mwezi Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeshafanyika kwenye mikoa 28 na kwamba mikoa ya Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga inatarajiwa kukamilisha zoezi hilo tarehe 07 Machi, 2025.

“Hadi leo tarehe 05 Machi, 2025 Tume imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 28. Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee. 

Aidha, zoezi la uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa wa Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga kwenye Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga unaendelea tangu tarehe 01 Machi, 2025 na utakamilika tarehe 07 Machi, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhan amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
 
“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura   4,071,337. Aidha, idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema Kailima.

Ameongeza kuwa mkoa wa Dar es Salaam una vituo    1,757   vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo      96     katika vituo         1,661    vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Kailima amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari linahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine.
 
“Uboreshaji wa Daftari pia utahusu kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo,” amesema Kailima.


Mwisho.

--
Mroki Mroki
Online Reporter/Blogger
Mob: +255 755 373999 
     DODOMA, TANZANIA

WIZARA YA UTALII ZANZIBAR YATOA MAFUNZO MAALUM KWA WATEMBEZA WATALII (BEACH BOYS)

 Na Ali Issa Malezo 4/3/2025.

Wizara ya Utalii na mambo ya Kale Zanzibar imewapatia mafunzo maalum watembeza watalii 150 (Beach Boys) ili kuona kazi hiyo inafanywa vizuri kwa kulinda maslahi ya Zanziabr na tamaduni zisipotee.

Yamesemwa hayo leo huko Maruhubi katika Chuo cha Hoteli na Utalii na Mkurugenzi wa Utalii Dkt. Abdallah Mohamed wakati alipokuwa akizundua mafunzo hayo ya siku tatu kwa vijana wanao tembeza watalii hapa Zanzibar.

Amesema utalii ni sekta muhimu Zanzibar ambayo unaongeza pato la Taifa na wananchi wengi kufaidika na sekta hiyo, hivyo kupatiwa vijana mafunzo hayo ni wajibu kwani kutapelekea mustakabali mzuri kwa watembaza watalii pamoja na kuilinda hazina hiyo isipotoshwe na kuharibiwa.

“Tunalinda hazina ya utalii zanzibar hatuwezi kuwaacha kufanya kazi kiholela usiharibiwe utalii isiharibiwe na tumebaini wapo baadhi ya watembeza watalii hawana taluma ya kutosha katika masuala ya tuor gaide,lakini wapo hawapo leseni (vitambulisho) wanafanya kazi kwa mazoea, hivyo mafunzo haya matarajio yetu kuona vijana hawa wanafanya kazi kwa ustadi mkubwa kuwahudumia watali”alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha alisema kuwa mafunzo hayo pia yatafanyika Pemba kwani Kisiwa hicho kinafunguka kiutalii.

Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo Ali Hassan Ali Afisa kutoka Wizara ya Utalii na mambo ya kale alisema kuwa taaluma wanayoitoa kwa vijana hao ni kuwajengea uwezo pamoja na kuifahamu Zanzibar na mazingira yake ikiwemo historia ya nchi, utamaduni wa watu wake na hali halisi ya watu wa Zanzibar walivyo bila ya kupoteza ukweli.

Aidha alisema kuwa Wizara imebaini wapo baadhi ya watembeza watalii hawana taaluma ya kutembeza watalii hivyo wakaona ipo haja ya kuwapatia mafunzo hayo.

Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Ali Omari Masoud amesema anashukuru kupata mafunzo hayo kwani yatawapa weledi wa kujua yale ambayo aliyokuwa hayajui na yatamjengea uwezo katika kazi zake.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamejumuisha watembeza watalii 150 ambapo mada mbalimbali zimeandaliwa ikiwemo kuzijuwa sehemu za hitoria ya Zanzibar, fukwe safi, hoteli kubwa, sehemu wanazo zipenda wageni na wanachohitaji wageni katika maeneo wanayo yatembelea.







Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aipongeza Mamlaka ya Mapato ZANZIBAR

Written By CCMdijitali on Saturday, March 1, 2025 | March 01, 2025

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Ofisi ya Zanzibar (TRA) kwa kufanikiwa katika ukusanyaji wa Mapato Nchini.
 

Ameyasema hayo katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Mlipa Kodi iliyofanyika katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mazizini Zanzibar. 

Mhe. Hemed amesema mafanikio yaliyofikiwa katika ukusanyaji wa mapato umetokana na mashirikiano yaliyopo Baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa kuwaweka karibu wafanyabiashara hali ambayo imepelekea wafanyabiashara hao kuwa wepesi katika suala la ulipaji wa Kodi. 

Aidha amesema TRA Ofisi ya Zanzibar imefikia mafanikio ya kuvuka malengo ya ukusanyaji wa kodi waliyopangiwa kutokana na ushirikiano mzuri  baina yao na walipa kodi ikiwa ni njia muhimu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo Wananchi wake. 

Amesema juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mapato na kuchochea Kasi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Miundombinu na utoaji wa huduma Bora kwa jamii. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka Uongozi wa TRA Zanzibar kuzidisha juhudi katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuongeza wigo wa walipakodi kwa kusimamia vizuri mifumo mbali mbali ya ukusanyaji wa mapato, kusisitiza maadili ya watendaji, kupambana na rushwa na kutoa huduma bora kwa walipa kodi. 

Mhe.Hemed amewahimiza watendaji wa TRA Zanzibar kuendelea kutoa elimu ya mlipa kodi ili kila mtu ajue faida ya kodi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Serikali kutoa huduma za kijamii kama vile maji safi na salama, afya,elimu, nishati ya umeme na nyenginezo. 

Aidha Mhe. Hemed amewahakikishia kuwa Serikali zote mbili zinatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ambao ndio wanaoiwezesha Serikali kutekeleza shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na kutoa huduma za kijamii. 

Sambamba na hayo amewahakikishia kuwa mapato yote yatokanayo na kodi yatatumika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wakubwa , wa kati na wadogo, pamoja na wawekezaji kwa ili kupunguza gharama za uwajibikaji na kuleta wepesi katika ulipaji wa kodi, kuongeza mapato, kukuza ajira na kuondoa umasikini Nchini. 

Amewataka wananchi wote kuendelea kulipa kodi na kudai risiti kila wanapopata huduma na watoa huduma wahakikishe wanatoa risiti kila wanapotoa huduma na kusisitiza kuwa Serikali haitamfumbia macho mtu yoyote atakaekwepa kulipa kodi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ili kukomesha vitendo hivyo visiendelee. 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Serikali kupitia Mamlaka za Mapato zinajipanga kuweka mazingira mazuri, wezeshi na rahisi kwa wafanyabiashara na walipa kodi nchini ili kuendelea kuwajenga kuwa na utayari wa kulipa kodi kwa wakati. 

Amesema jukumu la Serikali ni kuweka Sheria na kanuni Bora zitakazosaidia kuwawezesha walipa Kodi waweze kutimiza wajibu wao wa kulipa Kodi kupitia mifumo madhubuti iliyowekwa na Mamlaka za Mapato Tanzania. 

Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Ndugu Yussuf Juma Mwenda  amewapongeza wafanyabiashara Nchini kwa kuchangia kulipa Kodi kwa hiari hatua iliyopelekea kuwapatia tunzo kutokana na mchango wao Mkubwa katika kufikia malengo ya kukusanya Kodi Nchini. 

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka Mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara hatua ambayo imepelekea kuongezeka kwa wawekezaji na kutanua wigo wa Kodi Nchini Tanzania. 

Akitoa salamu kwa niaba ya sekta binafsi bwana Suleiman Ali Moh'd kutoka Taasisi ya Uwekezaji ya Utalii(ZATI) amesena Taasisi yake imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na TRA Zanzibar hasa katika suala zima la kutoa elimu na kuwaelimisha wawekezaji juu ya umuhimu wa kipa kodi kwa hiari. 

Amesema Taasisi binafsi zianatambua umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa hivyo, watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanalipa kodi kwa hiari na ndani ya wakati ili kupata maendeleo endelevu ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi zawadi ya Mshindi wa kwanza wa tunzo za walipaji kodi bora mwaka 2023/2024 kwa Wawakilishi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) katika hafla ya siku ya mlipa kodi iliyofanyika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort.






WAZIRI KOMBO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI, AAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO.

Written By CCMdijitali on Friday, February 28, 2025 | February 28, 2025

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amefanya ziara rasmi katika Ubalozi wa Tanzania jijini Lilongwe, Malawi, kwa lengo la kukagua miundombinu ya ubalozi huo, kupokea taarifa za maendeleo, na kusikiliza changamoto zinazokabili shughuli za kidiplomasia.

 

Katika ziara hiyo, Mhe. Kombo alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, pamoja na maafisa wa ubalozi, ambapo alipokea taarifa kuhusu hali ya mahusiano ya kidiplomasia, uchumi, siasa, na usalama kati ya Tanzania na Malawi.

 

Taarifa hiyo ilihusisha pia masuala ya mali za Serikali ya Tanzania zilizopo nchini Malawi, ustawi wa watumishi wa ubalozi, na mchango wa Watanzania waishio Malawi katika maendeleo ya taifa.

 

Aidha, Waziri Kombo alipokea maelezo kuhusu fursa mbalimbali zinazoweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, hususan katika uwekezaji, biashara za mpakani, na sekta ya utalii.

 

Akizungumza na maafisa wa ubalozi, Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kuitangaza vyema Tanzania kimataifa na kutumia fursa zilizopo kwa manufaa ya maendeleo ya taifa. Alitoa wito kwa Watanzania waishio Malawi kushirikiana na ubalozi katika kukuza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

 

Kwa upande wake, Balozi Agnes Kayola alimshukuru Waziri Kombo kwa ziara yake na kuahidi kuwa ubalozi utaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa maslahi ya Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akisoma kitabu cha taarifa cha Ubalozi alichopewa na Balozi wa Tanzania nchini Malawi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (katikati) akiwa na  Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola (kushoto) na kulia ni Mkuu wa Utawala David Fupi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisaini kitabu cha wageni kwenye makazi ya Balozi wa Tanzania nchini Malawi.



 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link