MAJALIWA: UBORA WA MIRADI UWIANE NA THAMANI YA FEDHA ZINAZOTOLEWA

  WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ya elimu kuhakikisha inakamilika kwa ...

Latest Post

MAJALIWA: UBORA WA MIRADI UWIANE NA THAMANI YA FEDHA ZINAZOTOLEWA

Written By CCMdijitali on Monday, January 6, 2025 | January 06, 2025


 
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ya elimu kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
 
Ametoa wito huo leo (Jumatatu Januari 06, 2025) wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Makoba iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar. Ufunguzi wa skuli hiyo ni sehemu ya shamrashamra kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
 
Amesema kuwa Serikali imeendelea kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa elimu ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
 
Aidha, Mheshimiwa  Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuipa hadhi sekta ya elimu kwa kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu.
 
“Sina shaka leo hii chini ya Jemedari Dkt. Hussein Ali Mwinyi sote tunashuhudia mwendelezo wa hatua kubwa ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini. Suala hili ni la kujivunia kwa kuwa ni Matunda ya Mapinduzi ambayo sasa yanafikisha miaka 61 tangu kuasisiwa kwake”.
 
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi, imeendelea kufanya mageuzi makubwa ya elimu katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu nchini. “Mageuzi hayo ni pamoja na kutekeleza mtaala mpya wa umahiri utakaomwezesha mtoto kujifunza kwa vitendo na kumudu kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia”.
 
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na kufanya jitihada za makusudi za kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwenye sekta zote za kijamii ili kuleta tija inayotarajiwa kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohamed Mussa amesema kuwa Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza ari ya Waasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha analeta mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu.
 
“Serikali hii iliahidi kuboresha miundombinu ya madarasa kwa shule za msingi kwa kujenga madarasa 1,000 na 500 kwa ngazi ya Sekondari na mpaka sasa kwa ngazi ya msingi imejenga madarasa 2,893 na ngazi ya Sekondari imejenga madarasa 1,917”
 
Ujenzi wa Shule hiyo ambao umefikia asilimia 100 umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.1 ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi.









DKT NCHEMBA AIPONGEZA TRA KUIMARISHA MAPATO



Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka sh. trilioni 22.2 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia sh. tril. 27.6 mwaka wa fedha 2023/2024 na kuvunja rekodi ya kukusanya sh. trilioni 16.528 katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 kinachoanzia Julai hadi Desemba Mwaka 2024.

Dkt. Nchemba alitoa pongezi hizo, wakati akifungua Kikao Kazi cha siku 5 kinacho Tathmini Utendaji kazi wa Nusu Mwaka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Jijini Arusha.

Alisema kuwa fedha hizo zimeisaidia Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za jamii kama vile Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, Mradi wa Treni iendayo kasi (SGR), miundombinu ya barabara, huduma za jamii na mingine mengi

Dkt. Nchemba aliitaka TRA kuimarisha zaidi mifumo ya kisasa ya kielektroniki ya kukusanya mapato ya Serikali ili kuongeza uwazi, tija na ufanisi kwa kukusanya mapato pamoja na kuziba mianya ya maafisa wa TRA kukutana uso kwa uso na walipakodi. 

Aidha, Dkt. Nchemba alirejea wito wake kwa Mamlaka hiyo kutofunga biashara za watu wanaowadai kodi badala yake waweke utaratibu wa kuzilea biashara hizo huku wakihakikisha kodi stahiki zinalipwa na wahusika kwa kuwa vitendo vya kufunga biashara vinaathiri uchumi wa nchi pamoja na kuvuruga mfumo wa biashara husika na kuwasababishia watu umasikini na kuwakosesha wananchi ajira.

Dkt. Nchemba alitumia wasaa huo pia kuwataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi, kutumia ipasavyo mashine za kukusanya mapato ya Serikali (EFDs) na kuwahimiza watoe risiti halali zinazoendana na thamani ya manunuzi yaliyofanyika huku wananchi kwa upande wao wakihimizwa kudai risiti halali wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.

Kwa upande wake, Kamisha Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema kuwa Kikao kazi hicho, pamoja na mambo mengine, kilikuwa na malengo kadhaa ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo waliyowekewa na Serikali ya kukusanya shilingi trilioni 30.449 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Alimhakikishia Mhe. Waziri wa Fedha, kwamba Mamlaka hiyo itafikia malengo hayo na pengine kuzidi kidogo kutokana na viashiria vya ukusanyaji mapato katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 ambapo hadi kufikia Desemba mwaka 2024, TRA imekusanya sh. trilioni 16.528, ikilinganishwa na makusanyo ya sh. trilioni 9.242, ya kipindi kama hicho  Mwaka 2020/2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 78.78.

Bw. Mwenda alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na TRA kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao hatua iliyochangia kukua kwa uhusiano kati ya Mamlaka na walipakodi hususan kupitia viongozi wa vyama vya wafanyabiashara wote nchini wanaoendelea kuunga mkono kwa vitendo  juhudi zinazofanywa na Serikali baada ya maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha mazingira ya biashara na ulipajikodi nchini.

Aliwahimiza watumishi wa TRA kuendelea kufanyakazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kukusanya mapato yake kupitia kodi mbalimbali pamoja na kuzingatia weledi wanapotekeleza majukumu yao wakati Serikali kwa upande wake ikiendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi.









RAIS MWINYI:TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI UDSM INA MCHANGO MKUBWA



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Taasisi ya Sayansi za Bahari  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ina Mchango Mkubwa katika Mipango na Sera  za  kuendeleza Uchumi wa Buluu unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la Msingi Jengo la Taaluma na Utawala la taasisi hiyo Buyu ,Wilaya ya Magharibi B ,Mkoa wa Mjini Magahribi.

Aidha Rais Mwinyi  ameahidi  Serikali kuendelea Kushirikiana na  Taasisi hiyo  wakati wote kwa lengo la kuhakikisha  Rasilimali za Bahari ziliyopo zinatumika ipasavyo ili kutoa Mchango Mkubwa kwa Uchumi na Ustawi wa jamii.

Amefahamisha kuwa kuimarika kwa  Miundombinu ya Taasisi hiyo hapa Zanzibar  kutatoa mchango mkubwa wa sekta nyengine muhimu  ziliyomo katika Uchumi wa Bulu .

Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa matarajio ya Serikali ni  kuona Sekta ya Utalii inayochangia asilimia 30 ya Uchumi wa nchi ,Uvuvi ,Ukulima wa Mwani  na Mazao ya Baharini zinaimarika  kupitia Tafiti zitakazoandaliwa na Taasisi hiyo pamoja kutoa Wataalamu wenye weledi watakaojifunza katika taasis hiyo.  

Amezitaja sekta nyengine  kuwa ni Bandari, Mafuta na Gesi  na Usafiri wa Baharini.

Ameyalezea Matarajio mengine kuwa ni kwa Taasisi hiyo  Kufanya Tafiti  za Uchumi wa Buluu  zitakazotoa  Matokeo bora kwa ajili  ya  Uandaaji wa Sera na Mipango ya Maendeleo ya Sekta hiyo. 

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia kwa  Mchango wao katika miradi mingi ya Maendeleo nchini      kitendo kinachoonesha Kuaminika kwa Serikali zote mbili za SMT na SMZ kutokana na Matumizi mazuri ya fedha za Miradi ya Maenďeleo na Kuwasisitiza kuendelea na Mchango huo.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi ametoa rai kwa Wawekezaji  kulitumia Eneo la Buyu kuchangamkia Fursa za  Uwekezaji  kutokana na Mandhari nzuri ya   eneo hilo  kwa Makaazi na Malazi kwa Wanafunzi ,Huduma za Usafiri ,Kumbi za Mikutano ,Huduma za Utafiti ,Hospitali , Utafiti wa Bahari na  Shughuli mbalimbali za Kijamii.














WAZIRI WA AFYA AKABIDHI VITENDEA KAZI KWA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII VYENYE THAMANI YA SHILINGI ZA KITANZANIA MILIONI 674.3

Written By CCMdijitali on Saturday, January 4, 2025 | January 04, 2025



Na WAF - Bukoba, Kagera

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amekabidhi vitendea kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii vyenye thamani ya Shilingi za kitanzania Milioni 674.3 kwa mikoa Saba ambayo ni  Njombe, Pwani, Kigoma, Ruvuma, Songwe, Lindi pamoja na Kagera. 

Waziri Mhagama amekabidhi vitendea kazi hivyo Januari 03, 2025 akiwa mkoani Kagera kama mwakilishi wa  mikoa mengine Sita itakayotoa huduma za afya kwa wananchi ikiwemo elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya milipuko. 

"Vitendea kazi vilivyokabidhiwa ni pamoja na viatu maalum vya kazi, miamvuli, mabegi pamoja na sare maalum zitakazowatambulisha  kuwa wao ni wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakaokuwa wawili katika kila kitongoji (mwanamke na mwanaume)," amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema, mpango huo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni mpango wa Taifa unaoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, shabaha likiwa ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 Tanzania iwe na wahudumu wapatao  137,294 nchi nzima ili kupunguza magonjwa. 

Aidha, Waziri Mhagama amesema katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassa, Serikali imewezesha uwepo wa dawa pamoja na vifaa tiba ikiwemo vifaa vya uchunguzi ambavyo vinatumia tekinolojia ya hali ya juu. 

"Sasa hivi kuna ongezeko la mashine ya uchunguzi wa magonjwa MRI 14, CT-Scan 45, Digital X- Ray 439, Ultrasound zaidi ya 600 pamoja na Pet-Sacan 1 mpya yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 18 ambayo tumeifunga pale kwenye Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya wagonjwa wa kansa," amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema vifaa hivyo vinahitaji wataalam wabobezi, hivyo Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa Shilingi Bilioni 30 ili kusomesha wataalam bingwa na wabobezi katika masuala ya afya ikiwemo madaktari bingwa wa mionzi na usingizi. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajat Fatma Mwasa ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Sekta ya Afya kwa uendelea kuboresha miundombinu pamoja na upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba ambavyo vimeweza kuwahudumia wananchi wa mkoa huo katika masuala ya afya. 

"Hospitali yetu ya Rufaa ya Bukoba inapokea wagonjwa zaidi ya 300 kwa siku kwakuwa tunao madaktari bigwa 12 wanaokidhi katika fani mbalimbali, tunatoa shukurani za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuimarisha huduma za afya kwa wagonjwa ikiwemo wagonjwa p, na kwa sasa hospitali yetu inatoa huduma kama zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili," amesema Mhe. Mwasa.






















 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link