.JPG) |
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa
Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co Ltd ya Korea Kusini baada
yeye na ujumbe wake kumtembelea ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini
Dodoma tarehe 30 Machi 2022. |
.JPG) |
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na ujumbe kutoka Korea
Kusini ulioongozwa na Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co
Ltd Munseok Lee baada ya kumtembelea ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali
Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Machi 2022. |
.JPG) |
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe
kutoka Korea Kusini ulioongozwa na Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions
Co Ltd Munseok Lee mara baada ya kumtembelea ofisini kwake eneo la Mji wa
Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Machi 2022. |
 |
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akimvisha vazi la kimasai Mtendaji
Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co Ltd ya Korea Kusini baada ya kumtembelea
ofisin ya Wizara ya Ardhi eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe
30 Machi 2022. |
WIZARA YA ARDHI YASHIRIKIANA NA KOREA
KUBADILISHA
MIFUMO YAKE KUWA YA KIDIGITALI
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ushirikiano
wake na Korea Kusini imeanzisha mkakati wa kuhakikisha inabadilisha mifumo yake
upangaji, utumiaji, upimaji na uwekaji kumbukumbu za sekta ya ardhi kutoka
analogia kwenda digitali ili kuboresha sekta ya ardhi.
Hatua hiyo inafuatia mifumo mingi ya upangaji, utumiaji upimaji
na uwekaji kumbukumbu za ardhi katika Wizara ya Ardhi kuendelea kutumia mifumo
ya analogia katika upangaji, utumiaji, upimaji na uwekaji kumbukumbu za sekta
ya ardhi.
Katika kufanikisha azma hiyo Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na
Serikali ya Korea Kusini zimeingia makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji
mradi wa ujenzi wa kituo cha Kisasa cha Mafunzo pamoja na uboreshaji
miundombinu ya sekta ya ardhi.
Hayo yamebainishwa tarehe 30 Machi 2022 jijini Dodoma na Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi wakati
akielezea ushirikiano baina ya serikali ya korea kusini na Wizara ya ardhi
katika uanzishaji kituo cha kisasa cha kutolea mafunzo kwa wataalamu wa upimaji
pamoja na uboreshaji miundombinu ya sekta ya ardhi.
Uanzishwaji Kituo cha kisasa utagharimu fedha
za kitanzania Shilingi Bilioni 5.2 na ule wa ujenzi wa miundombinu utagharimu
dola milioni 64.
Akielezea ujenzi wa kituo cha kisasa, Dkt Kijazi alisema
uanzishwaji wa kituo hicho siyo tu kwa ajili ya kutumia teknolojia ya kisasa
pekee bali ile itakayoendana na wakati ambapo kupitia mradi huo Wizara ya Ardhi
itapokea msaada wa kiufundi sambamba na wataalamu wake kupatiwa mafunzo na
kuwekewa vifaa vinavyohusu mifumo ya ardhi.
‘’Pamoja na kuwekwa vifaa kwenye kituo lakini pia watumishi
watajengewa uwezo pamoja na kukusanya, kuchakata na kutumia takwimu za ardhi
katika mipango ya kuendeleza sekta ya ardhi’’ alisema Dkt Kijazi.
Akigeukia sehemu ya pili ya mradi huo, Dkt
Kijazi alisema, itakuwa ni ujenzi wa miundombinu itakayowezesha wizara ya Ardhi
kutumia teknnolojia ya kisasa katika masuala mazima ya kupanga, kupima na
kutumia takwimu za ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi..
Mradi mzima utahusisha uandaaji ramani za uwiano mdogo na zile
za uwiano mkubwa kwa ile miji mikuu ya mikoa 26 ya Tanzania Bara sambamba na
kuweka vituo vya kielektroniki vya upimaji ardhi na kuboresha miundombinu ya
kusambaza taarifa za kijografia kwa idara za serikali na watumiaji wote nchini.
Katika hatua nyingine, ujumbe wa wataalamu kutoka Korea kusini
uliokuja kwa ajili ya hatua za awali za utekelezaji miradi hiyo ukiongozwa na
Afisa Mtendaji Mkuu wa Hojung Solution Co Ltd Munseok Lee umekutana na Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa ajili ya
kujitambulisha na kumuelezea maendeleo ya utekelezaji miradi hiyo.
Ujumbe huo ulimueleza Dkt Mabula uko tayari
kuanza kazi ya utekelezaji mradi huo baada ya maandalizi ya awali ya kutoa
mafunzo kwa baadhi ya watumishi nchini.
Kwa upande wake Dkt Mabula aliuambia ujumbe huo
kuwa ana imani ujumbe huo ulishiriki vyema hatua zake za awali za maandalizi ya
utekelezaji mradi huo na kueleza kuwa matarajio yake kila kitu kitaenda vizuri
katika utekelezaji mradi huo.